Yanga yakimbilia CAF kulidai bao la Aziz Ki

Muktasari:

  • Katika mechi hiyo ya marudiano iliyopigwa usiku wa jana kwenye Uwanja wa Luftus Versfeld, Pretoria Afrika Kusini, ilipata bao dakika ya 57 kupitia Aziz KI aliyefumua shuti kali lililogonga besela kabla ya kutumbikia langoni kisha kurudi uwanjani na mwamuzi kupitia VAR alilikataa.

Saa chache tangu Yanga itolewe katika mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa kwa penalti 3-2 na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, imeamua kukimbilia Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kudai bao la Stephane Aziz KI lililokataliwa na mwamuzi Dahane Beida.

Katika mechi hiyo ya marudiano iliyopigwa usiku wa jana kwenye Uwanja wa Luftus Versfeld, Pretoria Afrika Kusini, ilipata bao dakika ya 57 kupitia Aziz KI aliyefumua shuti kali lililogonga besela kabla ya kutumbikia langoni kisha kurudi uwanjani na mwamuzi kupitia VAR alilikataa.

Kitendo hicho kilifanya mchezo huo kumaliza dakika 90 timu zikiwa 0-0 kama ilivyokuwa katika mchezo wa kwanza wiki iliyopita jijini Dar es Salaam na kusababisha mechi kuamuliwa kwa penalti na Yanga kupoteza mikwaju mitatu kupitia Aziz KI, Dickson Job na Ibrahim Bacca.

Hata hivyo, mabosi wa klabu wakati wakiwa njiani kurejea nchini, tayari wameiandikia barua CAF kulalamikia maamuzi hayo wakiamini yalikuwa yana upendeleo kwa wenyeji na kuwepo kwa harufu ya upangaji wa matokeo wakikomaliza sheria ya CAF namba XVI.

Yanga imeliomba shirikisho hilo kufanya uchunguzi juu ya maamuzi yaliyofanywa na Beida lililoinyima timu hiyo ushindi halali na kutaka kujua kama kuna upangwaji wowote wa matokeo katika mchezo huo wa jana.

Katika barua hiyo, iliyosainiwa na Mwanasheria wa Yanga, Patrick Simon, Yanga ililalamikia timu nzima ya waamuzi ikiongozwa na Dahane Beida waliokataa bao la Stephane Aziz Ki lililofungwa dakika ya 57 ya mchezo wakiamini lilikuwa ni halali.

Vilevile imelalamikia kitendo cha VAR kutotumika kwa usawa unaotakiwa, kwani matukio mengi yaliyoonekana kuwa upande wa wapinzani yaliachwa kama lile la kutazama kadi nyekundu kwa Yanga halafu ikaacha kuamua goli la Aziz Ki.

Yanga imeitaka CAF kupitia tena mechi nzima na kurudia video za VAR na kuchukua hatua kwa wote watakaokutwa na hatia ya upangaji wa matokeo katika mchezo huo.

Mwanaspoti ilimtafuta Mwanasheria wa Yanga Patrick Simon ambaye alithibitisha ni kweli wamewasilisha malalamiko kwenda CAF.

"Ninachoweza kusema ni kwamba tumewasilisha malalamiko yetu CAF."

Ushindi iliyopata Mamelodi imeifanya ifuzu nusu fainali ikiungana na Al Ahly iliyoitoa Simba kwa jumla ya mabao 3-0 na sasa zinasubiri matokeo ya mechi za leo usiku ili kujua zitakutana na nani katika hatua hiyo.

Mechi zinazochezwa leo ni ile ya saa 1:00 usiku kati ya Petro Atletico ya Angola na TP Mazembe na mshindi ataumana na Al Ahly, wakati saa 5:00 usiku itakuwa ni zamu ya Asec Mimosas ya Ivory Coast itakayoialika Esperance ya Tunisia ili itakayosonga ikakutane na Mamelodi wanaoshikilia taji la AFL.