VIDEO: Boxer arejea Yanga, Zahera akomaa na Molinga

Muktasari:

Katika mazoezi hayo, Kocha Mwinyi Zahera alielekeza zaidi wachezaji kupiga pasi ndefu kutoka kwa viungo na kuwapa washambuliaji walioongozwa na David Molinga kufunga mabao.

Mwanza. Beki wa Yanga, Paul Godfrey ‘Boxer’ ametumia takribani dakika 120 kujifua peke yake ikiwa ni programu maalumu aliyopewa na Kocha Mkuu Mwinyi Zahera ili kujiweka fiti.

Godfrey alikuwa majeruhi kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya goti na enka sasa ameanza kufanya mazoezi ya uwanjani kabla ya kujiunga na wenzake.

Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Boxer alisema kwa sasa amekaa vizuri na yuko tayari kuanza kurudi kikosini.

Alisema sasa anasubiri uamuzi wa benchi la ufundi kumpa namba katika mechi ijayo dhidi ya Mbao FC.

Katika mazoezi hayo Yanga ilianza mazoezi saa 5:00 asubuhi na kumaliza saa 7: 11 mchana kwenye Uwanja wa Nyamagana.

Katika mazoezi hayo, Kocha Mwinyi Zahera alielekeza zaidi wachezaji kupiga pasi ndefu kutoka kwa viungo na kuwapa washambuliaji walioongozwa na David Molinga kufunga mabao.

Hata hivyo, Zahera alitumia muda mwingine kuzungumza na nyota wake haswa Molinga huku akifichua siri ya kufanya hivyo.

Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Zahera alisema hadi sasa anafurahia kiwango cha vijana wake na kwamba hata waliokuwa majeruhi anaona wanakuja vizuri na kwa ubora.

"Nilikuwa nazungumza nao ili kuwaelekeza jinsi ya kufanya, hata Molinga nilikuwa nampa mbinu jinsi ya kuomba mpira na namna ya kuwapita wapinzani na kufunga" amesema Zahera.

Ameongeza kuwa anaamini mazoezi waliyonayo yatawasaidia kupata ushindi katika mchezo ujao na kwamba wanafahamu wazi wanapokutana na Mbao huwa ni mechi ngumu kutokana na ushindani wanaoupata.

Ameeleza kuwa wanatarajia kutumia mchezo huo kujenga kujiamini kabla ya mechi ya kimataifa dhidi ya Pyramid na kwamba matarajio yao ni kushinda michezo yote.

"Tunafanya mazoezi yetu hatuwaangalii wengine,tunajua mechi ya Mbao itakuwa ngumu kutokana na rekodi yao kwetu,ila tutatumia mchezo huo kujiamini kabla ya kuwavaa Pyramid," alisema kocha huyo.

Mkongo huyo alisema ishu ya kujitokeza katika mchezo wa Mbao na Ruvu Shooting haikuwa na lengo la kuwafuatilia wapinzani hao, isipokuwa alienda kujipumzisha tu.

"Sikwenda kwenye mchezo wa Mbao na Ruvu kuwafuatilia wapinzani, nilienda kupoteza muda na kujiliwaza baada ya kutoka kulala, tunajipanga sisi kivyetu," alisema Zahera.