Gidabuday ang'oka RT, aaga akimtaja Mzee Ruksa

Muktasari:

Gidabuday akiwa katibu mkuu wa RT, Tanzania ilifanikiwa kutwaa medali mbili za shaba zilizoletwa na Alphonce Simbu kwenye mashindano ya dunia ya 2017 nchini Uingereza na Francis Damiano alishinda medali kwenye michezo ya Jumuiya ya madola kwa vijana mwaka huko Bahamas.

MIAKA mitatu ya Ukatibu Mkuu wa Shirikisho ya Riadha Tanzania (RT) kwa Wilhelim Gidabuday tangu alipochaguliwa Novemba 27, 2016 umekatika ghafla baada ya kujiuzulu na kumkabidhi madaraka Ombeni Zavalla, huku akiaga kwa kuwatolea mifano Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.
Gidabuday amejiuzulu nafasi hiyo ya Ukatibu baada ya kikao cha Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na wajumbe wa RT jana Ijumaa.
Katika kikao hicho kilichodumu kwa saa 3.30, Gidabuday aliamua kujiuzuru nafasi hiyo aliyoitumikia kwa miaka mitatu na miezi 11 huku akisisitiza hajajiuzulu kwa shinikizo bali kwa maslahi ya riadha nchini.
"Hata mzee Mwinyi kabla ya kuwa Rais aliwahi kujiuzulu Uwaziri, Dk Ndumbaro alifungiwa na TFF, lakini sasa ni Waziri," alisema Gidabuday alipokuwa akimkabidhi madaraka Zavalla ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa RT.
Alisema sababu ya kujiuzulu kwake ni moja tu, anataka maslahi mapana ya RT.
"Wote tunahitaji mafanikio lakini kila mmoja ana njia ya kuyafikia, hivyo naona njia yangu haikuungwa mkono na wengi," alisema kiongozi huyo huku akikanusha taarifa kuwa amejiuzulu ili akagombee ubunge wa jimbo la Hanan'g.
Naye Makamu wa Rais wa RT, William Kallaghe alisema Kamati ya Utendaji imebariki uamuzi wa Gidabuday na Mkutano Mkuu utakaofanyika mwezi ujao jijini Dodoma utaamua kuhusu nafasi ya Katibu Mkuu.
"Katika kikao cha Waziri, kila mjumbe wa RT alieleza anachokiona kwenye riadha, baadae tulikaa kikao cha kamati ya utendaji na Gidabuday kutangaza kujiuzulu.
"Kamati ilibariki uamuzi huo na kumteua Zavalla kukaimu nafasi hiyo sanjari na kuwateua Dk Hamad Ndee, Filbert Bayi na Juma Ikangaa ambao watapendekeza namna bora ya maandalizi ya timu yetu kuelekea kwenye Olimpiki ya 2020.