Rais RT amshtukia Gidabuday

Thursday December 6 2018

 

By Imani Makongoro

SHIRIKISHO la riadha Tanzania (RT) limesalia na siku 25 za mbichi na mbivu kufanya mashindano ya taifa mwaka huu, lakini baadhi ya wadau wake akiwamo aliyewahi kuwa Rais wa RT, Francis John wameshtuka.

Iko hivi, RT kupitia kwa Katibu wake, Wilhelim Gidabuday inasisitiza hata iweje lazima wafanye mashindano ya Taifa mwaka huu hasa baada ya mwaka jana kutofanyika.

Lakini aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa RT (sasa Rais), Francis John anakwambia kwa siku zilizosalia kabla ya mwaka kuisha hana uhakika wa kuwepo kwa mashindano hayo ambayo kama yasipofanyika athari zake ni kubwa kwa RT.

“Sidhani kama yatafanyika, bado kuna usiri katika kueleza ukweli kuhusu mashindano, kama yapo mbona RT hawasemi ni lini au tarehe ngapi yatafanyika,” alihoji Francis.

Alisema kuandaa mashindano ya Taifa siyo jambo dogo, linahitaji maandalizi ya kutosha na kwenye riadha timu shiriki mara nyingi zinalipiwa chakula na malazi na Shirikisho.

“Wacha tusubiri, lakini kwa siku zilizosalia, sina hakika kama tyatakuwepo, kilichopo ni RT kuandaa majibu ya kupeleka IAAF (Shirikisho la riadha la kimataifa) kueleza sababu za kutofanya mashindano ili kuepuka ‘rungu’ la IAAF,” ALISEMA.

Alitaja moja ya adhabu ambazo RT inaweza kukutana nazo kutoka IAAF kwa kushindwa kuandaa mashindano ya Taifa ni kukosa mgao wa fedha za Shirikisho hilo ambazo hutolewa kila mwaka. Hata hivyo, Katibu Mkuu, Gidabuday amesisitiza mashindano yatafanyika na RT inaendelea na maandalizi na lazima yafanyike.

“Wanaohoji mashindano watulie waendelee na maandalizi, tutafanya kama yalivyopangwa.”

Advertisement