Gidabuday: Mashindano ya Taifa ya riadha yako nje ya uwezo wangu

Muktasari:

Mwaka 2017, RT ilishindwa kufanya mashindano ya Taifa ambayo moja ya adhabu zake ni kufungiwa msaada kutoka Shirikisho la Kimataifa (IAAF) ambapo walionywa na mwaka 2018 walifanya mashindano ya Taifa huku mwaka huu tena wakiwa mguu ndani mguu nje kufanya.

Dar es Salaam.Wakati kukiwa na sintofahamu juu ya hatma ya mashindano ya riadha ya Taifa, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelim Gidabuday amesema suala hilo liko juu ya uwezo wake.

Msimu huu, RT imesogeza mashindano hayo mara kadhaa huku mara ya mwisho ikiwa Julai ambapo uongozi wa riadha ulitangaza kuyaahirisha wiki moja kabla ya tarehe iliyopangwa kufanyika.

Akizungumzia hatma ya mashindano hayo msimu huu, Gidabuday alisema kinachokwamisha ni ukosefu wa fedha, suala ambalo liko nje ya uwezo wake.

"Tulipanga bajeti ya Sh48 milioni ili kuyafanikisha, ambazo zilikuwa ni gharama za chakula, malazi na usafiri wa ndani kwa washiriki pamoja na medali kwa washindi.

"Bahati mbaya tumekosa fedha hizo, japo kuna mdau ametuahidi kutupati Sh42 milioni, lakini mpaka sasa bado hatujafanikiwa kuipata fedha hiyo," alisema Gidabuday.

Alisema amekuwa akipata usumbufu wa mara kwa mara kutoka kwa viongozi wa timu za mkoa ambazo zimeanza maandalizi ya mashindano kutaka kujua hatma ya wachezaji wao.

"Ishu inayotukwamisa ni fedha, hakuna kingine, timu zilishaanza maandalizi, lakini bahati mbaya hatuna fedha mkononi ya mashindano zaidi ya ahadi," alisema Gidabuday.