Riadha Tanzania inaangukia hapa

Muktasari:

Mtihani wao wa kwanza ulikuwa kwenye Olimpiki ya Rio 2016 nchini Brazil wengi wakisubiri ile ahadi ya kuchoma vyeti kama itajirudia.

MWAKA 2012, Wilhelim Gidabuday alijizolea umaarufu baada ya kuahidi kuchoma vyeti endapo timu ya riadha ya Tanzania ingerejea na medali ya Olimpiki iliyofanyika London, Uingereza.

Ahadi hiyo haikutimia, miaka miwili baadaye akashinda ukatibu mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania akimrithi Suleiman Nyambui ambaye alipata kibarua cha kuinoa timu ya Taifa ya riadha ya Brunei.

Novemba 2015, Gidabuday alichaguliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Riadha nchini kwenye uchaguzi mkuu akimpiku nyota wa zamani wa mbio ndefu, Gidamis Shahanga.

Ujio wa Gida kama anavyojulikana kwenye tasnia ya riadha, ulifufua matumaini mapya akishirikiana na Rais Anthony Mtaka na makamu wake, William Kalaghe na wajumbe wengine.

Mtihani wao wa kwanza ulikuwa kwenye Olimpiki ya Rio 2016 nchini Brazil wengi wakisubiri ile ahadi ya kuchoma vyeti kama itajirudia.

Mafanikio yaanza

Mwaka 2016 ulikuwa wa mafanikio kwenye riadha ambapo Alphonce Simbu aliingia kwenye orodha ya wanariadha watano bora wa marathoni kwenye Olimpiki, mwaka 2017 Tanzania ilishinda medali ya shaba ya dunia na medali kama hiyo kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola kwa vijana iliyoletwa na Damas Damiano.

Haikuishia hapo, wanariadha Failuna Abdi, Gabriel Geay, Agostino Sulle na Simbu waling’ara katika mbio za mialiko za kimataifa nje ya nchi.

“Tulishirikiana, kila kiongozi alitoa mchango wake katika kuhakikisha riadha inasonga, tulikuwa na pesa, lakini mambo yamebadilika sasa, RT haina ushirikiano tena,” anasema Gidabuday.

Mwaka huu Tanzania imechemka kwenye mashindano ya dunia nchini Qatar, wanariadha, Failuna Abdi, Stephano Huche na Agostino Sulle walishindwa kumaliza mbio za marathoni wakati Simbu aliyekuwa akitetea medali yake ya shaba akimaliza wa 16.

Licha ya joto kali nchini Qatar kutajwa kuwa chanzo, Gidabuday anasema hiyo si sababu kubwa, tatizo lilikuwa ni maandalizi ambayo RT haikutimiza wajibu wake.

Tatizo lilianza hivi

“Walianza vizuri mno mwaka 2016 hadi 2017, wadau walijitokeza kuidhamini riadha, kila mmoja alikuwa na fikra za mafanikio lakini sasa mambo ni kama yanakwenda ndivyo sivyo,” anasema Nyambui.

Anasema Katibu wa RT amekuwa kama jeshi la mtu mmoja ndani ya shirikisho, jambo ambalo katika mchezo wowote ule haliwezi kufanikisha kama watendaji hawawajibiki.

Nyota mwingine wa timu ya Taifa, Gidamis Shahanga anasema RT hakuko shwari japo kuna usiri wakijaribu kuficha hali hiyo, lakini ushirikiano wa miaka miwili iliyopita sasa haupo.

“Hata timu ilipoagwa kwenda Qatar ilionekana kama wamekata tamaa,” alisema nyota huyo ambaye picha yake iliwahi kutumika kwenye stampu enzi anakimbia.

Gidabuday anakiri hali hiyo akifafanua kwamba kwenye kamati yao wako zaidi ya 20, lakini hakuna aliyeshiriki hata kuaga timu zaidi yake yeye ambaye alikuwa miongoni mwa wanaosafiri na ofisa habari wao, Tullo Chambo na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Dk Hamad Ndee ambaye alitoa udhuru.

“Achilia mbali kuaga, hakuna aliyeshiriki kujua timu itafikaje Qatar, IAAF (Shirikisho la Riadha la Kimataifa) lilikuwa linalipia usafiri, lakini hadi timu inapokuwa kule ndipo wana kurefund (kurejeshea pesa uliyotumia),” anasema.

Anasema kama sio Simbu kumuomba meneja wake mzungu awadhamini kwenye tiketi ili IAAF watakapowapa pesa wakalipe basi timu ingekwama kuondoka.

Ishu yote iko hivi

Gidabuday anasema katika uongozi wao sasa, ule ushirikiano uliokuwapo kabla ya Olimpiki ya 2016 na mashindano ya dunia ya 2017 haupo tena.

Japo hakutaka kuweka wazi ni mambo gani hayaendi sawa, mtendaji huyo anasema idadi kubwa ya watendaji ni kama wamelisusa shirikisho.

“Kuna haja ya Serikali kuingilia kati, kuna tatizo kubwa RT, natamani kumuona Waziri wa Michezo na kumueleza hili, ili atusaidie mambo yakae sawa.

Hata hivyo, baadhi ya wajumbe wa kamati ya utendaji ambao wameomba hifadhi ya majina yao wamesema mpasuko unaoendelea RT umekwamisha mambo mengi.

Mmoja wa wajumbe alimtuhumu Gidabuday kuwa chanzo cha mpasuko huo akisisitiza kuwa tatizo kubwa ni Katibu Mkuu kufanyia uamuzi masuala ya shirikisho peke yake.

“Yeye (Gidabuday) ndiye analeta ukiritimba wa uongozi, yeye kama katibu masuala yote ya shirikisho lazima aitishe kamati tendaji, lakini vikao haitishi tutafanyaje?,” alihoji.

Mjumbe mwingine anadai chama kimekuwa kikiendeshwa na watu wawili na hata hafla ya kuaga timu iliyokwenda Qatar kwenye mashindano ya dunia (ilifanyika Arusha) hawakushikishwa zaidi ya kuishia kuona kwenye televisheni.

“Tunashangaa Tullo sijui yeye anaendaje, chama kimebaki cha Gidabuday na Tullo, katibu amekuwa na uamuzi wa peke yake bila kuishirikisha kamati tendaji,” alisema.

Tullo anasema sio kweli kwamba shirikisho linaendeshwa na watu wawili ambao ni katibu na yeye, akisisitiza hata wengine pia wanashirikishwa, lakini naye amethibitisha kuwapo kwa mgogoro wa kiuongozi.

“Katika uongozi kutofautiana kupo, ni kweli kuna kusigana kati ya viongozi, lakini hayo ni masuala ya kuzungumzika kwenye kamati tendaji yakaisha.

“Ni mambo ambayo tunaweza kuyasovu na kuishia ndani ya kamati tendaji na kazi zikaendelea na si kuyatoa nje,” anasema.

Mjumbe mwingine ambaye pia aliomba hifadhi ya jina alidai wana zaidi ya mwaka na nusu kamati ya utendaji haijawahi kukaa vikao.

“Ili kusigana kuishe kuna haja ya kuitisha kikao cha dharura na kuwekana sawa, vinginevyo hali itazidi kuwa mbaya,” alisema.

“Katibu ndiye mtendaji, lakini yeye ndiye anakuwa kikwazo hivyo Shirikisho linaonekana kulegalega, ni ngumu sana kusonga mbele,” anasema.

Gidabuday anasema yeye ataonekana mbaya kwa kuwa anasimamia ukweli.

“Siwezi kusema hii ni nyeusi wakati naiona ni nyekundu, labda hilo ndilo tatizo langu.

“Lakini RT sasa kuna kuoneana sana, kama nakomolewa, lakini siku nitalifikisha suala hili kwa Waziri wa Michezo, wizara yake ije ituchunguze kama mimi ndiye kikwazo au nani?,” alisema.

Alidai licha ya kususiwa timu, lakini amebeba jukumu la kuhakikisha inakwenda Qatar kwenye mashindano ya dunia mwaka huu.

“Simbu alibeba dhamana ya kuisaidia RT dola 1,500 ya kulipa visa na bima, alituombea pia kwa meneja wake akatuwekea dhamana ya tiketi kwenda Qatar,” anasema Gidabuday.

Nini kifanyike?

Katibu wa Chama cha Riadha mkoa wa Arusha, Alfredo Shahanga anasema ili mambo yaende sawa, uongozi kwanza unapaswa kuwa kitu kimoja.

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Riadha mkoa wa Mara, Daniel Thomas anasema, RT ijitafakari upya, lakini pia iondoe ukabila kwenye mchezo huo ili mambo yaende.

Nyambui anasema kikubwa ni viongozi kuwa kitu kimoja na kufanya kazi kwa ushirikiano kuwe na utaratibu wa vikao vya kamati ya ufundi na utendaji. “Hii itasaidia,” anasema.