Dante, Yanga bado hakijaeleweka

Muktasari:

Baada ya kupewa siku saba Mwanaspoti lilipenyezewa kwamba uongozi huo ni kama umeendelea kuchukulia poa kwa kutozungumza na mchezaji huyo lolote.

SAKATA la madai kati ya beki wa Yanga, Andrew Vicent ‘Dante’ na uongozi ni kama limetanda wingu, baada ya uongozi kuendelea kumpotezea licha ya kupewa muda wa kumalizana na Kamati ya Hadhi, Sheria ya Shirikisho la Soka (TFF).

Uongozi wa Yanga na msimamizi wa mchezaji huyo ulikutana Jumamosi iliyopita katika kikao cha Kamati, Hadhi, Sheria na Wachezaji ili kumalizana, lakini haikuwa hivyo.

Mabosi wa Yanga walipoenda katika kikao hicho kwa mara ya kwanza Oktoba 18, walipewa siku 14 wamalizane naye, lakini ilishindikana na ndipo wakakutana tena Novemba 2, lakini bado waliomba kuongezewa siku saba za kujishauri na kupitia upya madeni ambayo wanadaiwa.

Baada ya kupewa siku saba Mwanaspoti lilipenyezewa kwamba uongozi huo ni kama umeendelea kuchukulia poa kwa kutozungumza na mchezaji huyo lolote.

Katika kikao chao kilichofanyika Oktoba 18, uongozi ulipewa sharti la kulipa pesa za usajili wa Dante nusu kwa msimu uliopita, huku kwa msimu huu wakilipa kwa mafungu matatu kiasi cha Sh54 milioni.Baada ya vuta ni kuvute hiyo, Mwanaspoti jana Ijumaa lilimtafuta ofisa habari wa Yanga, Hassan Bumbuli aeleze kuhusu ukimya huo, lakini aligeuka mbogo.

“Leo (jana) sisi tuna mechi akili yetu ipo katika mechi, sasa hizo siku saba sisi za nini.” alisema na kukata simu.

Hata hivyo mmoja wa wana kamati ya Hadhi, Sheria na Haki za Wachezaji alisema: “Kesho (leo) Jumamosi siku saba ndio zinamalizika, kwa hiyo baada ya hapo ndio tutajua tunafanyeje, Yanga waliomba kupitia upya madeni yao kwa hiyo tunasubiri kuona watasema nini kwanza, wasipokuwa na majibu ndio tutajua tunafanya nini.”

Kwa upande wa kesi zingine zinazohusiana na masuala ya soka, alisema, “kesi nyingi zimeshamalizika baada ya pande zote kueleweka.”