Hersi, Kamwe wageuka kivutio Yanga

Muktasari:
- Watatu hao wamesimama na kucheza nyimbo mbalimbali zilizopigwa ukiwemo Aviola baada ya gari hiyo kusimama zaidi ya nusu saa kutokana na foleni.
Rais wa Yanga Hersi Said, ofisa habari wa klabu hiyo Ally Kamwe na kiungo mshambuliaji Clatous Chama wameibuka washehereshaji kwa kucheza juu ya gari lililobeba mataji ya klabu hiyo.
Watatu hao wamesimama na kucheza nyimbo mbalimbali zilizopigwa ukiwemo Aviola baada ya gari hiyo kusimama zaidi ya nusu saa kutokana na foleni.
Msafara wa Yanga ulitoka uwanja wa ndege 13:15 na kukaa zaidi ya nusu saa maeneo ya Tazara ambapo hadi saa 15:03 lilisimama kwa muda kupisha magari mengine kutoka barabara tofauti na uliopo msafara.
Chama ambaye amejiunga na Yanga dirisha kubwa la usajili akitokea Simba amevalia jezi nyeusi na kaptula nyeusi kichwani alitupia kofia nyeupe na kujitanda bendera ya Yanga begani.
Watatu hao baada ya kucheza wamepiga picha ya pamoja na kutulia kusubiri foleni imalizike ili waweze kuendelea na msafara.
Yanga inafanya paredi baada ya kufanikiwa kutwaa makombe matano msimu huu, Kombe la Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la CRDB, Kombe la Toyota, Kombe la Muungano na Ngao ya Jamii.