Prime
Kwaheri 2024-2025 umetufumbua macho, kuzibua masikio

Muktasari:
- Naomba tutumie nguvu zote kuuaga huo msimu wa 2024-2025 na tuombe utusaidie kutafuta suluhisho la matatizo makubwa yaliyokuwa yamejificha na tuombe sana yasijirudie tena.
SI jambo la kawaida msimu wa soka kuisha kwa mechi moja tu ya Ligi Kuu kuchezwa, huku orodha kamili ya majina ya timu zitakazocheza Ligi Kuu na Ligi ya Championship haijawa kamili na bingwa wa Kombe la Shirikisho kupatikana siku tatu baadaye.
Naomba tutumie nguvu zote kuuaga huo msimu wa 2024-2025 na tuombe utusaidie kutafuta suluhisho la matatizo makubwa yaliyokuwa yamejificha na tuombe sana yasijirudie tena.
Mechi zilizotakiwa kuhitimisha msimu wa Ligi ya 2024-25 zilichezwa Juni 22, huku watani wa jadi, Simba na Yanga, waliokuwa wameshikilia karata ya bingwa, wakicheza mechi za kutimiza wajibu siku hiyo. Wakubwa hao walimalizia msimu ulioanza Septemba kwa kukutana Juni 25 baada ya mechi ya Machi 8 kukumbwa na mizonga mingi.
Kutofanyika kwa mechi hiyo ya Machi 8 ndio kulisaidia kuchokonoa vitu vingi vilivyokuwa vimejificha. Simba ilitishia kugomea mechi hiyo kwa madai, ilizuiwa kufanya mazoezi ya mwisho Machi 7 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Hali ikijua kuwa dosari hiyo haifikii kiwango cha kuahirisha mechi, Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, ikaamua kuahirisha mechi hiyo tofauti na msimamo wake awali kuwa mechi ingechezwa kama ilivyopangwa.

Ikatumia kanuni inayoipa mamlaka ya kuahirisha mechi ‘kwa jinsi itakavyoona inafaa’ lakini haikutekeleza wajibu wa kupata haki ya kutumia kanuni hiyo, au kuthibitisha sababu za msingi zinazoweza kusababisha waone inafaa kuahirisha mechi.
Yanga ikagomea ikasema lazima ipeleke timu uwanjani kwa kuwa uahirishaji haukufuata kanuni na kwamba wapinzani wasipokuja itadai pointi tatu. Ikafanya hivyo na huo ukawa mwanzo wa mgogoro uliochukua miezi mitatu hadi mkuu wa nchi alipoziita pande zote na kuzitaka kumaliza tofauti zao na mchezo uchezwe.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPLB), Steven Mnguto aliandika barua ya kujiuzulu na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wake, Almasi Kasongo, alisimamishwa na Rais wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Wallace Karia, ambaye Yanga ilisema ni lazima ajiuzulu pamoja nao.
Uamuzi huo ulikuwa ni kati ya matakwa ya Yanga ili ikubali kucheza mechi ambayo ingepangiwa tarehe mpya, huku jambo moja la kushinikiza katibu mkuu wa TFF aondoke likiwa halijatekelezwa.
Lakini kabla ya kufikia uamuzi huo wa wawili hao kuliibuka mechi iliyofumbua macho ya wadau wa mpira.
Kwamba, kumbe bodi haina mfumo wa kuwawajibisha viongozi wake wakuu hadi vyombo vya TFF vishughulikie! Yaani mambo mengine yanahitaji kamati ya utendaji ya TFF na mengine mkutano mkuu wa TFF, kwa mujibu wa majibu ya Kasongo alipozungumza na waandishi kuhusu takwa la Yanga kuhusu wawili hao kuondolewa TPLB na bodi hiyo kuwa huru.

Kwa maneno mengine, mkutano mkuu wa klabu ambao hufanyika kila baada ya msimu kumalizika, hauwezi kuunda mfumo unaoweza kuwapa uhuru wa kujifanyia mambo yao wenyewe kama makusudio ya kuanzishwa chombo hicho yalivyokuwa na kanuni za uendeshaji zilivyo.
Kumbe Kamati ya Uongozi ya TPLB haiwezi kuchukua hatua zozote dhidi ya viongozi wakuu iwapo watakuwa wamefanya makosa? Sasa Kamati ya Uongozi ya TPLB ina kazi gani kama si kuwekwa kama sanamu?
Kumbe Mwenyekiti wa TPLB ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Bodi ya Ligi na ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi? Nani anamwajibisha kama anahusika kila sehemu, akiwa na cheo hichohicho?

Hapo kuna dhana ya utawala bora kweli? Nani atamuwajibisha mwenzake? Chombo gani kitakiwajibisha kingine? Mbona ni mfumo wa kiimla sana?
Hivi Mnguto, ambaye si mwenyekiti tena wa Coastal Union, aliendelea kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Ligi kwa sifa gani ikiwa hata makamu mwenyekiti wa klabu haruhusiwi kuongoza chombo hicho kwa nafasi ya mwenyekiti?
Kumbe uahirishaji mechi kiholela ulishakuwa utamaduni? Kumbe mechi ya Yanga na Simba ni ya tatu (kwa zinazojulikana) kubadilishwa kwa jinsi hiyo.
Ukiacha mechi iliyobadilishwa muda wa kuanza kiholela misimu mitatu iliyopita, kumbe TPLB iliwahi kuahirisha mchezo wa Kagera Sugar na Simba kwa mtindo huo wa ‘jinsi itakavyoona inafaa’ saa chache kabla ya kuanza kwa mchezo baada ya Simba kusema wachezaji wake wanaumwa mafua?

Kumbe Bodi ya Ligi imerudi nyuma kimuundo kuliko ilivyokuwa wakati inaanzishwa? Yaani, badala ya kusonga mbele na kuimarisha muundo na kupata watendaji wanaoendana na kiwango cha sasa cha ligi hiyo, bado wenyeviti na wawakilishi wa klabu ndio wanaingia kwenye kamati zake kama ile ya uongozi, ambako kumejaa kuoneana aibu.
Kumbe benki ya CRDB, inayodhamini mashindano ya Kombe la Shirikisho, haikutangaza itatoa kiasi gani kwa mshindi baada ya kuchukua mashindano hayo katikati kutoka kwa Azam Media?
Kumbe benki hiyo hutoa fedha za mshindi mapema lakini washindi hawapewi hadi wenyewe wanaamua kuelekeza zitumike kulipia ada za wachezaji wa kigeni? Yaani TFF haina mfumo wa kudhibiti malipo ya klabu hadi izuie fedha za zawadi? Inawezaje kuzuia wachezaji wa Tabora United wasicheze mechi ya Ligi Kuu hadi wakamilishe taratibu za usajili, ikashindwa kuzuia wachezaji wa Yanga kucheza hadi walipiwe ada? Au huu ndio msaada ambao Yanga ilipewa?
Inawezekanaje CEO wa Bodi ya Ligi akawa anawajibika kwa rais wa TFF? Ni mfumo gani huo wakati TPLB ina Kamati ya Uongozi? Kwa maneno mengine ni kwamba watendaji wa Bodi ya Ligi ni waajiriwa wa TFF? Inawezekanaje chombo kinachoendesha ligi ya nne kwa ubora Afrika yenye klabu zenye bajeti ya hadi Sh10 bilioni, ikawa hawawezi kutafuta watendaji wanaolingana na mazingira inayoyaona kila siku katika uendeshaji na usimamizi.

Ukiacha ‘kumbe’ zilizoibuliwa na sakata la mechi ya Machi 8, bado kuna mengi yaliyotokea msimu huu. Tangu msimu uanze hadi unaisha mijadala haikuwa utamu wa ligi, bali makosa ya waamuzi.
Kila raundi ilipoisha, vyombo vya habari na wadau waliona zaidi makosa kuliko uzuri, utamu wa mechi, ujanja wa wachezaji, ufundi wao, mbinu za makosa na menginbe yanayoufanya mchezo wa mpira wa miguu upachikwe jina la “our beautiful game (mchezo wetu mzuri)”. Huyo aliyebuni jina hilo angeangalia msimu ulioisha wa Tanzania, sijui angeupa mchezo huu jina gani?
Kudhihirisha na kubariki hoja kwamba waamuzi wetu wana matatizo, mechi ya Juni 25 ya Simba na Yanga iliamuliwa na waamuzi kutoka Misri. Kumbe hatuna mkakati wa kuboresha uamuzi hadi tukaweka upenyo wa kutumia waamuzi wa kigeni pale tutakapozidiwa?
Ziko ‘kumbe’ nyingi zilizoibuka msimu ulioisha lakini hizo chache zimegusa maeneo kadhaa ambayo tunatakiwa tuyaangalie kwa macho mawili wakati huu tukijiandaa kwa msimu mpya. Bado kuna mageuzi makubwa yanahitajika kuupeleka mpira wetu kule kunakostahili na hayo hayatawezekana bila ya juhudi za kila mmoja anayeweza kuchangia.