Dante aibana Yanga, Samatta naye aiponza Simba SC

Muktasari:

Kesi hizo zinazohusiana na madai mbalimbali ya wachezaji zilikuwa zikisikilizwa na Kamati ya Sheria, Haki na Hadhi za Wachezaji chini ya mwenyekiti, Elius Mwanjala na makamu wake Zacharia Hans Poppe.

JANA Jumamosi ilikuwa ni mwendo wa kupishana tu kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Watu walikuwa wakiingia na bahasha mkononi, ambapo walalamikaji na walalamikiwa katika madai mbalimbali walitinga kusikiliza mashauri yao huku beki Andrew Vincent ‘Dante’ akiibana Yanga wakati usajili wa Mbwana Samatta ukiwatikisa Simba.
Kesi hizo zinazohusiana na madai mbalimbali ya wachezaji zilikuwa zikisikilizwa na Kamati ya Sheria, Haki na Hadhi za Wachezaji chini ya mwenyekiti, Elius Mwanjala na makamu wake Zacharia Hans Poppe. Kamati hiyo ilianza kusikiliza kesi hizo saa 6 mchana ambapo ya kwanza ilikuwa ya mchezaji wa Azam FC, Paul Peter anayelalamikiwa na aliyekuwa meneja na kocha wake, Liston Katabazi kuwa alisajiliwa kwenye timu hiyo bila kufuata utaratibu.
Kesi hiyo ilifunguliwa mwaka jana ambapo, kwa sasa inadaiwa pia kutinga ndani ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Kanda ya Kinondoni ambako viongozi wa Azam wametakiwa kwenda ili kuitikia wito.
Azam FC kwenye kesi hiyo iliwakilishwa na mkurugenzi wao mtendaji, Abdulkarim ‘Popat’ Amin ambaye alisema mchezaji wao alisajiliwa kutoka timu ya Mugabe FC.
Popat alifika kwenye ofisi hizo mapema sambamba na mlalamikaji, Katabazi wakisubiri kuitwa kusikiliza kesi hiyo.
“Leo (jana) tuliambiwa tulete nyaraka za malipo ya kumsajili huyu mchezaji ambapo tumeleta pamoja na barua. Tulilipa Sh1 milioni kuilipa hiyo timu na usajili wake ulikuwa ni Sh6 milioni,” alisema Popat.
 “Hivyo kamati imemtaka mlalamikaji alete vielelezo vyote ambavyo alivitumia kama gharama za kumtunza mchezaji huyo ili sasa waone cha kuamua kwani, ndivyo vitaeleza ukweli.” 
Mbali na Popat, pia wengine waliotinga kweye ofisi hizo ni wachezaji wa Yanga, Vincent Dante na beki wao wa zamani ambaye ni meneja wa sasa, Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Mwanaspoti ambalo lilikuwepo kwenye ofisi hizo lilimshuhudia Cannavaro alitua mapema akisubiri kuitwa huku akisema anaidai Yanga zaidi ya Sh10 milioni za usajili alipokuwa anaichezea.
Kwa upande wa Dante, kabla ya kuingia kusikiliza kesi yake alisema yupo tayari kucheza Yanga, lakini hadi haki yake ipatikane kama walivyokubaliana.

ILIVYOKUWA
Saa 7:08 mchana, Dante na Cannavaro waliitwa kusikiliza kesi yao ambapo ndani ya kikao hicho mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji Tanzania (Sputanza), Musa Kisoki alikuwepo. Baada ya muda mfupi wachezaji hao walitoka huku ikidaiwa kuwa kesi yao imeahirishwa baada ya ya uongozi wa Yanga kuomba siku saba kutokana na mabadiliko ya uongozi yaliyofanywa klabuni hapo.
Mwanjala, ambaye aliongoza kikao hicho aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Kiufupi Yanga wameomba siku saba ili kusikiliza shauri lao, kwani kuna mabadiliko ya kiuongozi wameyafanya.”

Mshahara wa Dante
Sakata la Dante na Yanga limekuwa gumzo kwa muda mrefu sasa huku beki huyo akiendelea kuweka msimamo wa kutoichezea hadi alipwe fedha zake za usajili, lakini inadaiwa anachukua mshahara kama kawaida. Habari za kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho zinasema Dante alikiri kuchukua baadhi ya malipo kama mishahara kutoka Yanga.
“Ni wazi hata yeye amekiri kuchukua mshahara, hivyo wanasubiri hizo siku walizoomba Yanga kuona nini kitaamuriwa,” kilisema chanzo hicho.
Habari zaidi zinasema kwamba beki huyo pamoja na wanaomsimamia walikubaliana na Yanga alipwe kwa awamu tatu kiasi cha Sh54 milioni anazodai, jambo ambalo Yanga wameshindwa kutekeleza.
Geita Gold
kurudisha timu?
Misimu miwili iliyopita Geita Gold ilishushwa daraja baada ya tuhuma za upangaji matokeo, lakini msimu uliopita wameshiriki Ligi Daraja la Kwanza baada ya kuinunua klabu ya Mshikamano FC. Makubaliano yalikuwa ni kuilipa Mshikamano Sh75 milioni jambo ambalo halijafanywa hadi sasa na uongozi wa timu hiyo ulifungua mashtaka kwa mambo mawili - walipwe pesa zao ama warudishiwe timu yao.
Kikao hicho kilidaiwa kutoa maamuzi mawili kwa uongozi wa Geita Gold wakiitaka kulipa pesa yote ama kurudisha timu. Kama timu itarudi ina maana kwamba Geita Gold itarudi madaraja ya chini ilikoshushwa awali.
Katibu mkuu wa Mshikamano FC, Playgod Matemba alisema kikao kimeamua kuwa wataandikiwa barua.
“Tuliuza kwa vile tulishindwa kuiendesha, lakini Geita hawajatulipa ndio maana tumekuja hapa. Hivyo tuko tayari kurudishiwa timu kama watashindwa kulipa pesa, hivyo tunasubiri kuona hiyo barua kwa sababu suala hili lina muda sasa,” alisema Matemba.
Simba nako kuna moto
Harakati hizo za jana hazikuiacha Simba salama ikidaiwa pesa kwenye dili la kumuuza straika matata wa Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta.      
      Kiongozi wa Jack Academy ambako alitokea Samatta aliliambia Mwanaspoti kuwa: “(Samatta) alipokwenda Mazembe (DRC) tulipewa kiasi cha fedha na Simba kama ilivyo makubaliano ya kimkataba, lakini alipokwenda Genk hawajatulipa wakati wenyewe wameshalipwa.
“Nadhani watatulipa kama tulivyokubaliana kwa kuwa ni haki yetu. Kiasi cha fedha tunachopaswa kulipwa ni siri yetu bado, kikubwa tulipwe pesa yetu,” alisema Mataifa ambaye alipoitwa kwenye kikao hakukaa hata dakika tano.

Mbao, Singida United
Hawa nao walikuwa na balaa lao wakidaiwa fedha za usajili na wachezaji.
    Mbao FC inashitakiwa kwa kutomlipa Raphael Siame anayedai Sh7 milioni huku kamati ikiahidi kuikata timu hiyo fedha hizo juu kwa juu.
Kwa upande wa Singida United wanadaiwa mkwanja na kiungo wao Nizar Khalfan.
Kamati hiyo ilimaliza kikao chake saa 10.40 jioni ambapo, maamuzi mengine yatatangazwa hapo baadaye.