Ishu ya Dante, Yanga kazi ipo kweli

Muktasari:

Uongozi wa Yanga uliwaandikia Dante na Juma Abdul barua ya kuwataka wajieleze kwa nini walishindwa kujiunga na kambi ya timu hiyo na wachezaji hao kila mmoja alijitetea kwa upande wake

UKIMYA wa madai ya pesa za usajili wa mchezaji Andrew Vicent ‘Dante’ na klabu yake ya Yanga unahitimishwa leo baada ya viongozi wa klabu hiyo kukutana.
Viongozi wa Yanga wanatarajia kukutana leo na kuzungumzia juu ya hatma ya mchezaji wao huyo ambaye amekosekana tangu katika maandalizi ya msimu mpya.
Mwanasheria wa beki huyo pamoja na viongozi wa Yanga walikutana na kuzungumza lakini Viongozi wa Yanga walimwomba mwanasheria wa mchezaji awape muda mpaka jana Jumamosi watakapokutana wao kama wao ili waweze kuzungumzia suala lake.
Awali, uongozi wa Yanga uliwaandikia Dante na Juma Abdul barua ya kuwataka wajieleze kwa nini walishindwa kujiunga na kambi ya timu hiyo na wachezaji hao kila mmoja alijitetea kwa upande wake.
Baada ya kujibu barua hiyo, uongozi ulimwita Dante na kutaka wampe pesa nusu lakini mchezaji huyo aliwataka wasubiri mpaka msimamizi wake arejee nchini, lakini baada ya kurejea uongozi umekuwa ukizunguka juu ya kukutana na wasimamizi wa mchezaji huyo.
Mmoja wa watu wa karibu aliliambia Mwanaspoti Mwanasheria wa mchezaji huyo amekuwa akienda makao makuu ya klabu hiyo bila mafanikio kabla ya juzi Ijumaa kuombwa wakutane Jumamosi.
“Mwanzo walikuwa wazito baada ya Mwanasheria kwenda pale mara kwa mara tangu walivyorudi kutoka Botswana, lakini hivi sasa wameambiwa kesho (leo) Jumamosi, ngoja tuone,” alisema.
Mwanaspoti linafahamu mchezaji huyo baada ya kukaa pembeni akiwa na matatizo ya kifamilia ya kuuguliwa na mama yake, uongozi hawakumwingizia pesa yake ya mshahara huku wachezaji wengine wakifanyiwa hivyo.
Dante anaidai Yanga zaidi ya Sh45 milioni zikiwa ni fedha za usajili baada ya kuongeza mkataba baada ya ule wa awali (miaka miwili) aliosaini akitokea Mtibwa Sugar kumalizika.