Dante, Yanga bado hakijaeleweka kabisa

Muktasari:

Uongozi unajitahidi kumaliza suala lake ili aweze kurejea kambini kwa sababu ni mchezaji wetu

Dar es Salaam. Beki wa kati wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’ bado amelivuruga benchi la ufundi la timu hiyo wakimtaka kambini huku mwenyewe akiweka mgomo alipewa chake japo kidogo ili mambo katika familia yake yaende.

Ule mzozo baina ya beki huyo na mabosi wake bado haujapatiwa ufumbuzi, kwani mazungumzo baina yao hajapata muafaka licha ya kuonekana dalili za wazi huenda Dante akaungana na wenzake kama atatekelezewa mahitaji yake.

Dante hakujiunga na timu hiyo tangu mwanzoni mwa msimu huu baada ya kudai fedha yake ya usajili ambayo hakulipwa sehemu yoyote ya pesa hiyo, huku Kocha Mwinyi Zahera akitajwa kumhitaji beki huyo kambini ili aungane nao kwenye safari ya Zambia wakifua awe fiti kama wenzake.

Baada ya mara kwa mara Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Fredrick Mwakalebela kusema wanamalizana na mchezaji huyo hali imekuwa tofauti huku siku zikizidi kwenda.

Mwakalebela ameweka wazi baada ya awali kuwa na mazungumzo na mchezaji huyo mambo yalikuwa yakiingiliana, lakini hivi sasa wapo katika hatua nzuri.

“Awali tulikuwa tukipanga hivi, lakini mambo yakawa tofauti kutokana na vitu vidogo vidogo kuingiliana, lakini kuanzia sasa Uongozi unajitahidi kumaliza suala lake ili aweze kurejea kambini kwasababu ni mchezaji wetu,” alisema Mwakalebela na kuongeza;

“Walimtafuta kwa njia ya simu na kuzungumza naye wakikata waonane lakini mchezaji huyo alikuwa yupo Vikindu. Tulitaka aende kambini kujiunga na wenzake, lakini alisema yupo Vikindu ana matatizo ya kifamilia, upande wa pesa tutampa nusu nusu kama ambavyo wenzake walivyopata.

Naye Dante alikiri kupigiwa simu na kiongozi wa Yanga wakizungumza aweze kujiunga na wenzake kambini.

“Kweli nilipigiwa simu na kiongozi (Jina Kapuni) aliniambia anataka kunifuata niende kambini, lakini niliwaambia kwamba wanipe kiasi kidogo cha fedha ambacho tulikubaliana baada ya kuniweka wazi kwamba mambo yao sio mazuri kwahiyo nasubiri,” alisema Dante.

Aliongeza yeye yupo tayari kurejea kambini na ndio maana amekuwa yupo kwenye mawasiliano ya karibu na Viongozi wake.

“Nafanya mazoezi kila siku kwa sababu hii ndio kazi yangu, kwahiyo nasubiri kuona namna ambavyo watakamilisha hili tulilokubaliana mara yaa mwisho,” alisema Dante.