Sinema ya Dante, Yanga imekaa vibaya kweli

Muktasari:

Nadhani Dante yamemkuta kwa vile labda hana anayemsimamia na kumpa ushauri mzuri katika kudai haki zake Yanga, aidha nao Yanga itakuwa inakosea kama inampuuza Dante aliyeipigania timu katika kipindi kigumu.

YANGA ipo jijini Mwanza na kesho Jumanne ilitarajiwa kuvaana na Toto Africans katika mchezo wa kirafiki.

Katika mchezo wa kwanza dhidi ya Pamba maarufu kama ‘TP Lindanda’ ilimalizika kwa sare bao 1-1.
Tuachane na hayo, Yanga ipo Mwanza ikijiandaa na mchezo wao wa kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco United ya Zambia.
Ni mchezo wa awali wa raundi ya kwanza, baada ya kila moja kupenya katika mechi za raundi ya awali. Yanga iliing’oa Township Rollers ya Botswana, wakati Zesco inayonolewa na Kocha wao wa zamani George Lwandamina iliitoa Green Mamba ya Eswatini.
Mechi hiyo itapigwa wikiendi ijayo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya Yanga kwenda Zambia kwa mechi ya marudiano itakayopigwa Uwanja wa Levy Mwanawasa, mjini Ndola.
Katikati ya maandalizi ya mechi hiyo, beki wao kisiki, Andrew Vincent ‘Dante’ hayupo na timu. Hajajiungana na wenzake tangu mwanzo mwa msimu huu. Kisa kikielezwa ni shinikizo la kutaka alipwe fedha anazoidai klabu hiyo ikitajwa kiasi cha Sh45 milioni.
Sakata la Dante, mmoja wa nyota walioipigania timu hiyo msimu uliopita wakati klabu ikiwa na hali mbaya kiuchumi na kuifanya imalize nafasi ya pili, linafanana na lile la Juma Abdul na Kelvin Yondani.
Hata hivyo, wenzake hao baada ya mgomo baridi tayari wameshajiunga na timu ikielezwa wamemalizana na viongozi,  huku taarifa nyingine zikisema wameshalipwa chao.
Mkasa huu hautofautiani sana na ule wa aliyekuwa kipa wa timu hiyo, Beno Kakolanya ambaye kwa sasa yupo Msimbazi baada ya TFF kuingilia kati kupitia kamati zake.
Kakolanya naye alikuwa na shinikizo kama hilo, akajikuta kwenye wakati mgumu mbele ya Kocha Mwinyi Zahera na mwishowe wakafikishana katika kamati za TFF na ndoa yao ikavunjwa rasmi.
Juzi kati nilimsikia mmoja wa viongozi wa Kamati ya Usajili ya Yanga akizungumzia sakata hilo. Alikuwa akizungumza kama shabiki wa soka tu na sio kiongozi anayetambua na kuthamini thamani ya wanasoka wetu.
Namna alivyokuwa akieleza mkasa huo wa Dante alishindwa kabisa kujitofautisha na wale mashabiki wanaozungumza kwa jazba wanapotoa maoni juu ya jambo fulani.
Binafsi nilishtuka kumsikia kiongozi huyo akitoa kauli hiyo dhidi ya Dante, lakini papo hapo nikarejea kwa beki huyo na kubaini naye pia amechemsha kudai haki zake akiwa nje ya timu.
Kususa timu kama shinikizo la kutaka kulipwa mara nyingi huja kumbana mchezaji, hata kama ni kweli anakuwa hatendewi haki na klabu mbaya zaidi, yeye ni mzawa tu.
Naam, lau angekuwa ni mchezaji wa kigeni hata majibu ya uongozi yasingekuwa ya hivyo na pengine suala hilo lingeshatatuliwa mapema.
Ukweli Ndivyo Ulivyo. Kumekuwa na kasumba ya muda mrefu ya kuwanyenyekea wageni na kuwapuuza wazawa, ilihali hawa ni vijana wetu. Ni watoto wetu wenyewe na ndugu zetu ambao wanaishii kwa kutegemea soka.
Wazawa wamekuwa rahisi kusajiliwa kwa mali kauli kulinganisha na wageni. Pia hata wachezaji wetu nao hawajitambui na wamekuwa wakijirahisi sana mbele ya viongozi, ndio maana wanaburuzwa kama watoto wadogo ilihali ni watu wenye familia zinazowategemea huko makwao.
Mgeni hawezi kutoka kwao kuja kucheza katika klabu zetu kwa ahadi ya kulipwa baadaye fedha zake ama mishahara. Hakuna! Bahati nzuri wenyewe wana upeo mpana, wanajitambua na wanacheza soka kwa akili, huku wakiwa na wanasheria wenye kuzijua kazi zao wanaowasaidia kwenye matatizo kama haya.
Kadhalika, hata wao wenyewe wanaisoma vyema na kuielewa mikataba kabla ya kusaini.
Hawaburuzwi ovyo na wakizinguliwa kidogo hawachelewi kusikia wamefika CAF kama sio Fifa kudai chao.
Kitu ambacho hata wazawa wanapaswa kuamka sasa, vinginevyo wataendelea kunyanyasika licha ya msaada mkubwa wanaotoa kwa klabu wanazozichezea.
Nadhani Dante yamemkuta kwa vile labda hana anayemsimamia na kumpa ushauri mzuri katika kudai haki zake Yanga, aidha nao Yanga itakuwa inakosea kama inampuuza Dante aliyeipigania timu katika kipindi kigumu.
Kwa zile kauli za kiongozi yule ni kama wanamkomoa kwa ule usemi wa ukimwaga ugali nasi twamwaga mboga, hii sio sawa!
Hata kama ni kweli Dante kachemka kwa kuamua kuigomea timu, bado viongozi wa Yanga wanapaswa kuheshimu mchango wa beki huyo, sambamba na kuangalia namna ya kumlipa haki yake.
Inawezekana Dante amechukua hatua hiyo baada ya kuona labda wenzake waliokuwa wakidai kama yeye wakitekelezewa, huku yeye akipuuzwa, lakini bado ingependeza aendelee kudai haki yake kwa kufuata taratibu akiwa pia yupo kazini.
Ni sawa tu na alichokisema Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alipozungumzia sakata hilo akidai uongozi wao unalifanyia kazi, akitofautiana na yule jamaa wa usajili.
Dante, anaweza kuendelea kupiga kazi, huku akishinikiza alipwe haki yake hata ikiwezekana kushtaki Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ama kwingineko anakodhani kutampatia jasho lake. Kuamua kubaki nyumbani kunaweza kumbana kisheria, lakini kupitia sakata hili kuna somo kwa wachezaji wengine na hata viongozi wanaosimamia klabu na soka la Tanzania kwa ujumla.
Wachezaji kupenda kwao kujisimamia kila kitu wakati mwingine ni mzigo, pia kuingia mkataba na klabu bila ya wanasheria ama wasimamizi na hata kuisoma na kuilewa imekuwa mateso kwao. Pia hata kukubali kwao kusajiliwa ama kufanyishwa kazi kwa mali kauli ni kujishushia hadhi zao. Warejee alichowahi kukifanya Mbwana Samatta alipokuwa Simba. Samatta aliigomea Simba akitaka apewe gari aliloahidiwa kwenye mkataba la sivyo wamsahau. Licha ya vitisho na mikwara ya mabosi wa Msimbazi, Samagol alikomaa na mwishowe alipewa chake na kurejea uwanjani na kuibeba Simba kabla ya kuonwa na TP Mazembe katika muda mchache aliyoitumikia timu hiyo. Wachezaji wasipojitambua na kujithamini wenyewe hakuna wa atakayewathamini na kuwajali. Lakini, ifike wakati wachezaji na viongozi waheshimiane na kutambua kila mmoja anamhitaji mwenzake, waiheshimu mikataba ama makubaliano wanayoingia kwa manufaa ya soka kwa ujumla.
Nao wasimamizi wa soka waangalie namna ya kuweka kanuni zitakazovibana klabu zinazokiuka mikataba na makubaliano ya haki za wachezaji, kwani kwa sasa imeanza kuwa ni donda ndugu.
Kadhalika kipo Chama cha Wachezaji Soka Tanzania (SPUTANZA), ni vyema kikapewa nguvu na wachezaji wakachangamka kujiunga kuwa wanachama ili kupata misaada kwenye sakata kama hizo.
Naamini kabla ya wachezaji kupewa ushauri wa ovyo, kupitia Sputanza wangeepushwa mapema kuingizwa chaka, kwani chama kingewasimamia kila hatua ya mikataba na hata pale inapokiukwa kama ilivyo sasa, ndio maana nawakumbusha wasikipuuze nacho pia kisilale kijitangaze vyema ili wachezaji wakikimbilie.
Lakini yote kwa yote ni kwamba pande mbili, yaani klabu ya Yanga na Dante wanapaswa kulimaliza jambo hili kiungwana, kwani wagombanao ndio wapatanao, pia kukomoana huwa hakujengi!