Beki Simba aipa tano Fifa

Muktasari:

Simba imecheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Bandari (ilishinda bao 1-0), Mashujaa (1-0), jambo ambalo Shamte analiamini linawajengea uwezo mzuri wa kushindana.

Dar es Salaam. Beki wa Simba, Haruna Shamte amesema mechi za kirafiki zitawaweka katika mazingira mazuri ya kufanya vyema kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ligi Kuu imesimama wiki mbili kuipisha Taifa Stars inayojiandaa kucheza na Sudan katika mchezo wa kufuzu Fainali za Chan Ijumaa wiki hii.

Simba imecheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Bandari (ilishinda bao 1-0), Mashujaa (1-0), jambo ambalo Shamte analiamini linawajengea uwezo mzuri wa kushindana.

“Mechi za kirafiki ni nzuri zinakuwa zinaonyesha mapungufu yapo wapi na kumfanya kocha kurekebisha kikosi chake mapema na kukiandaa kilicho bora,”

“Pia ndani ya kikosi chetu kuna ushindani wa namba, hapo ndipo pakuonyesha jitihada zote ili kumshawishi kocha,” alisema.

Alisema lengo kubwa ni kuendeleza ushindi ambao waliuanza ligi kuu na walishinda mechi nne.

“Ndio kuna wachezaji ambao wameitwa Stars, hivyo sisi tunatakiwa kuwa kwenye piki ili tukianza ligi tuendeleze ushindi ambao tulianza nao kwani huwezi kujua wapinzani wetu wanajipangaje,” alisema.

Simba ilishinda mechi za ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar (2-1), Kagera Sugar (3-0), JKT Tanzania (3-1) na Biashara (2-0), hivyo kufikisha pointi 12 kwenye msimamo.