Ujanja wote wa Shamte hapindui kwa Shemsa

Muktasari:

Shemsa anasema mume wake anapokuwa mapumziko anakuwa anahakikisha anamsimamia programu yake ya mazoezi anayokuwa anafanya asubuhi na jioni, akidai siku akitaka kutegemea basi anakuwa mkali

WAHENGA hawakukosea waliposema nyuma ya mafanikio ya mwanaume yupo mwanamke. Neno hilo linaishi kwa beki wa Simba, Haruna Shamte anayekiri kila hatua ya maendeleo yake ya soka mke wake, Shemsa, amehusika.
Mwanaspoti lilimtafuta Shemsa ili kujua ana mchango gani kwa Shamte, ambapo amefunguka mengi na jinsi ambavyo anapenda mume wake awe mfano wa kuonyesha kazi bora itakayokuwa mfano kwa wengine.
Ameyataja majukumu muhimu anayoamini yanalinda kiwango cha Shamte na kwamba, anapoona analegalega kuyatimiza basi anakuwa mkali na masihara huyaweka pembeni.
 
MFUATILIAJI WA MAZOEZI
Shemsa anasema mume wake anapokuwa mapumziko anakuwa anahakikisha anamsimamia programu yake ya mazoezi anayokuwa anafanya asubuhi na jioni, akidai siku akitaka kutegemea basi anakuwa mkali.
“Akirudi mapumziko namwambia anipe programu yake ya mazoezi, hivyo nakuwa naseti muda wa kumkumbusha ama kumuamsha asubuhi kwa sababu najua wazi kwamba hiyo ndio kazi ambayo itatakiwa tujenge maisha yetu, siwezi kufanya mzaha hata kidogo,” anasema.   

SHAMTE ANAPIGWA PINI
Kama kuna jambo halipendi Shemsa kutoka kwa mume wake ni kumuona anazurura bila mpangilio, hivyo anakuwa anamwambia apate muda wa kupumzika na ye kufurahia mapenzi yao.
“Najua kazi yake inatumia nguvu, ndio maana sipendi nimuone anazurura bila sababu, hilo nalichukia na huwa namwambia awe anapata muda wa kupumzisha mwili wake ili akirejea kazini anakuwa na uwezo mpya.
“Pia inakuwa ndio muda wa kufurahia mapenzi yetu kwani muda mwingi anakuwa mbali na familia, ninachoshukuru Mungu ni msikivu ingawa hilo la kuzurura nakuwa nalivalia njuga hadi anakuwa anaelewa namanisha nini.”

AKIWA NA WAKATI MGUMU
Anatambua kwamba soka lina changamoto nyingine na kwamba anapokuwa anaona mume wake anapitia magumu ya kumuumiza anakuwa karibu naye kuhakikisha haondoki kwenye mstari.
“Kazi ya mke ni kuhakikisha mume wake anakuwa kwenye afya njema ya akili kwa maana ya kumfanya asiwe na mawazo, namjua akiwa na furaha na huzuni, nikiona anapitia magumu basi namwambia maneno ya kumtia moyo.
“Nakuwa makini kujua ni vitu gani havipendi basi nakuwa naviepuka sana, ilimradi tu changamoto zisimuondoe kwenye kufanya kazi zake bora, namshauri kujituma bila kukata tamaa, amekuwa akinisikiliza,” anasema.

ANAFURAHIA MAPENZI
Shemsa anasema Shamte ni mwanaume anayejua mke anahitaji nini na anakuwa anavifanya kwa moyo bila kusukumwa, jambo linalomfanya ajione yupo ulimwengu mwingine kwenye mapenzi.
“Hakuna raha kama mwanaume anajua mahitaji yako, kiukweli mapenzi yetu hayajawahi kuchuja kila ninapomuona mume wangu namfurahia ingawa anapokuwa kambini nakuwa namkubuka sana uwepo wake, ila kwa kuwa ni kazi nakuwa namsisitiza aifanye kwa umakini mkubwa,” anasema.
“Ninachokipenda sana kwake nikimwambia unatakiwa kuongeza bidii katika kazi yako nakuwa naona mabadiliko, kifupi ni mume bora na baba bora wa mtoto wetu ambaye kwa sasa ana miezi mita no.”

Anasema safari ya mapenzi yao ilianzia mbali akidai walikutana mtaani kwao na baada ya kusomana tabia na kila mtu kuridhika na mwenzake wakaamua  kuuona.

“Hatuja- kurupuka kuoana tumeanza mbali nikapenda tabia zake na yeye akapenda zangu basi tukaamua kuishi pamoja na sasa tuna mtoto wa kiume ana miezi mitano,” anasema mwanamke huyo ambaye huwambii kitu  kwa Shamte.