VIDEO: Masaa mawili ya kesi ya Fei Toto, Yanga

Muktasari:
- Shauri hilo leo Alhamisi lilianza kusikilizwa saa 5:20 Asubuhi na kumalizika saa 7:20 mchana ambapo pande zote mbili ziliondoka eneo la tukio, katika ofisi za TFF Karume, Dar es Salaam.
KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), imetumia muda wa masaa mawili kumaliza kupitia upya shauri la mchezaji Feisal Salum ‘Fei Toto’ na klabu ya Yanga linalohusiana na mkataba baina ya pande hizo mbili.
Shauri hilo leo Alhamisi lilianza kusikilizwa saa 5:20 Asubuhi na kumalizika saa 7:20 mchana ambapo pande zote mbili ziliondoka eneo la tukio, katika ofisi za TFF Karume, Dar es Salaam.
Hayo yalikuwa mapitio ya pili baada ya mwanzo TFF kuamuru kuwa Fei Toto ni mchezaji halali wa Yanga na anapaswa kurejea kikosini lakini upande wa mchezaji huyo haukukubaliana na majibu hayo na kuomba mapitio ‘Review’ ambayo yamefanyika leo.
Katika mapitio hayo upande Feisal umemuongeza wakili Fatuma Karume kwenye jopo na kuungana na Makubi Kanju, upande wa Yanga yenyewe ilisalia na jopo lile lile la mwanzo chini ya Mkurugenzi wa Sheria wa klabu hiyo, Patrick Simon.
Hata hivyo, mawakili wa Yanga , Fei Toto sambamba na wale wa TFF hawakutoa jibu la mwisho juu ya shauri hilo na kusema TFF itatoa taarifa kamili muda wowote kuanzia sasa.
Ikumbukwe Yanga ilipeleka shauri kwenye kamati hiyo ikimtaka Feisal kutoa maelezo kwanini ameondoka ndani ya kikosi hicho na kuandika barua ya kuaga akiichapisha katika ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Desemba 24,2022 bila mazungumzo ya pande zote mbili.
Akiongea na Mwanaspoti, Wakili wa Feisali, Fatuma, alisema kila kitu kimeenda sawa na sasa wanasubiri jibu la mwisho huku akiitaka kamati ya TFF kupitia vyema mikataba hiyo.
“Kila kitu kimeenda vizuri na sasa tunasubiri majibu ya kamati hivyo tunawaomba wapitie kwa umakini jambo hili,” alisema Fatuma.
CEO wa Yanga, Mtine alisema hawana presha na wanasubiri jibu la mwisho tu.
“Tuliitwa kwenye review na tumekuja, tumesikilizwa na kusikiliza na sasa tunasubiri jibu la kamati tu,” alisema Mtine.
Ilivyotafutwa kamati ilisema itatoa majibu kamili ya kila kitu muda wowote kuanzia sasa.