Prime
Yanga yasaka saini ya kiungo wa Gor Mahia

Muktasari:
- Yanga inayoshikilia ubingwa wa Ligi Kuu kwa msimu wa tatu mfululizo, huku kwa sasa ikiongoza msimamo kwa tofauti na pointi moja dhidi ya watani wao wa jadi, Simba imepanga mechi ijayo itakayoikaribisha Dodoma Jiji ipigwe kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar.
YANGA imesharejea jijini Dar es Salaam na ilikuwa ikijiandaa kwenda Zanzibar kwa ajili mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji kabla ya kuweka kambi visiwani humo kusubiri Dabi ya Kariakoo ya Juni 25, huku mabosi wa klabu hiyo wakiendelea kufanya usajili wa kimyakimya kwa kikosi kijacho.
Yanga inayoshikilia ubingwa wa Ligi Kuu kwa msimu wa tatu mfululizo, huku kwa sasa ikiongoza msimamo kwa tofauti na pointi moja dhidi ya watani wao wa jadi, Simba imepanga mechi ijayo itakayoikaribisha Dodoma Jiji ipigwe kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar.
Mabosi hao wameamua mara baada ya mechi hiyo ya Jumapili ya wiki hii, itasalia huko huko kujiandaa na pambano la Dabi ya Kariakoo lililoahirishwa mara mbili, Machi 8 na Juni 15, lililopangwa sasa kupigwa Jumatano ijayo ya Juni 25 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Lakini ikiwa imesaliwa na mechi tatu za kufungia msimu ikiwemo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) litakalopigwa Juni 29 dhidi ya Singida Black Stars, klabu hiyo imedaiwa imetuma ofa ya kumnasa kiungo mkabaji Enoch Morrison anayekipiga Gor Mahia ya Kenya anayeelezwa kuwa mbadala sahihi ya kiungo Mganda, Khalid Aucho ambaye anamaliza mkataba, huku akiwa anasumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara, japo hivi sasa amerejea na bado ni tegemeo kikosini.
Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema mchezaji huyo kutoka Gor Mahia ni mmoja wa watakaovaa uzi wa kijani na njano msimu ujao, kwani mazungumzo ya pande zote mbili yanaelekea pazuri, ingawa mabosi wa Jangwani wamefanya siri katika utaratibu wa kuunda jeshi jipya la msimu ujao kimyakimya.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kililiambia Mwanaspoti kuwa Yanga inataka huduma ya mchezaji huyo kwa ajili ya kuimarisha eneo la kiungo na anatajwa kuwa ni nyota anaweza kuvaa kwa ufasaha viatu vya Aucho hata akikosekana licha ya kikosini kwa sasa kuwa na viungo wengine.
“Kwa sasa tegemeo ni Aucho, na anaonekana amechoka kutokana na kucheza mechi nyingi, anahitaji msaidizi, Mudathir Yahya yeye anapewa kazi ya kwenda kushambulia mianya inayoachwa na wapinzani, mara chache anakuja kumsaidia,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Eneo hilo pia lina Duke Abuya ambaye pia ameingia katika mfumo kwa kupata dakika za kucheza lakini hao wote ambao ndio wachezaji wa kutumainiwa kikosi cha kwanza hawana mikataba itakapofika mwisho wa msimu na haijajulikana nani atabaki nani ataondoka.”
Chanzo hicho kiliongeza kuwa endapo watafanikiwa kumalizana na kiungo huyo mwenye umri wa miaka 25, wataongeza damu changa eneo hilo na wanaelewa ubora wake hivyo itakuwa chachu ya kutengeneza kiungo mwingine bora ambaye atahudumu kikosini hapo kwa muda mrefu. “Hesabu za Yanga ni huyu, umri na kipaji chake ndio vilivyouvutia uongozi kumshawishi ili aje kuvaa uzi wa kijani na njano msimu ujao,” alisema mtoa taarifa.
Ujio wa kiungo huyo utamfanya aingie vitani na nyota ambao tayari wameandika rekodi ndani ya kikosi hicho licha ya mikataba yao kuelekea ukingoni ambao ni Aucho, Mudathir na Abuya nyota ambao wana vita ya kucheza kikosi cha kwanza.
Nyota wengine wanaocheza eneo hilo na hawana uhakika wa namba katika kikosi cha kwanza ni Jonas Mkude ambaye pia mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu, Aziz Andabwile ambaye yupo kwa mkopo na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Yanga inasaka taji la Ligi Kuu kwa msimu wa nne mfululizo sasa baada ya awali kulibeba mara tatu tangu ilipoipokea Simba iliyolibeba mara nne mfululizo na zote mbili zinachuana katika msimu huu, vijana wa Jangwani wanaongoza ligi kwa pointi 76 dhidi ya 75 za Wekundu wa Msimbazi.
Timu hizo Jumapili hii kila moja itakuwa nyumbani kumaliza mechi za raundi ya 30 kabla ya kuvaana Jumatano ijayo katika kiporo cha Dabi ya Kariakoo kilichoahirishwa mara mbili, Machi 8 na Juni 15 ambapo mshindi wa pambano hilo huenda akatangazwa bingwa wa msimu huu.
Yanga itakuwa wenyeji wa Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar wakati Simba itaikaribisha timu iliyoshuka daraja ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam na kila moja ikitaka angalau kudumisha tofauti ya pointi moja iliyopo.