TFF: Feitoto bado mali ya Yanga

LEO Machi 2, 2022 ilikuwa siku ya kamati ya Sheria na hadhi za wachezaji ya TFF kufanya mapitio ‘review’ ya kesi ya mchezaji Feisal Salum ‘Fei toto’ dhidi ya klabu ya Yanga kuhusu mkataba wa pande zote mbili na baada ya kila kitu kufanyika, TFF imetoa majibu kuwa Mchezaji huyo bado mali ya Yanga.
Yanga ilipeleka shauri kwenye kamati hiyo ikimtaka Feisal kutoa maelezo kwanini ameondoka ndani ya kikosi hicho na kuandika barua ya kuaga akiichapisha katika ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Desemba 24, 2022 bila mazungumzo ya pande zote mbili.
Baada ya hapo shauri hilo kwa mara ya kwanza lilisikilizwa na pande zote tatu (Kamati, Yanga na Feisal) Ijumaa ya Januari 6 mwaka huu na baada ya hapo TFF ilitoa barua iliyoeleza Feisal bado ni mchezaji halali wa Yanga kimkataba na kutoa nafasi ya upande wa Feisal kuomba mapitio 'Review’ kama hawataafiki jibu hilo.
Hata hivyo upande wa Feisal kupita kwa mawakili wake wakiongozwa na Nduruma Majembe na Makubi Kanju hawakukubaliana na majibu ya TFF na kuomba review ambayo ilipangwa kusikilizwa Februari 27, kabla ya kuahirishwa tena na kusikilizwa leo, Machi 2 na Yanga kushinda tena.
Mwanaspoti lilikuwa mubashara katika ofisi za TFF na kufuatilia kila kitu na kubwa zaidi ilikuwa ongezeko la Wakili maarufu, Fatuma Karume kwa upande wa Feisal na kuwa moja ya mawakili waliosikiliza shauri hilo kwa muda wa masaa mawili kuanzia saa 5:20 asubuhi hadi saa 7:20 mchana.
Baada ya hapo, kamati hiyo ya TFF ilijifungia ndani na kujafili muafaka na baadae kutoa barua iliyoeleza kuwa Feisal bado ni mchezaji halali wa Yanga.
Barua hiyo ya TFF imeeleza baada ya kusikiliza hoja zote za mawakili wa pande zote mbili (Yanga na Feisal) imeona kuwa shauri hilo la mpitio ‘review’ halina msingi wa kisheria kushawishi kamati kubadili maamuzi ya kamati yaliyotolewa awali na hivyo kamati imetupilia mbali shauri hilo.
Aidha Kamati hiyo imeeleza sababu za kiundani kuhusu shauri hilo zitatolewa kwa pande zote mbili zinazohusika katika shauri hilo (Feisal na Yanga), Siku ya Jumatatu Machi 6, 2023.
Usikose kujipatia nakala yako ya gazeti la Mwanaspoti kesho Machi 3, 2023 kwa taarifa zaidi juu ya sakata hilo.