Fatuma Karume atinga na Fei Toto TFF

Muktasari:
- Awali Fei Toto alisimamiwa na mawakili Nduruma Majembe na Makubi Kanju lakini leo wameonekana kuongeza nguvu kwa kumuongeza Fatuma kwenye jopo hilo na wakili huyo ndiye ametinga makao makuu ya TFF, Karume akiambatana na kiungo huyo.
LEO Machi 2,2023, ndio siku ya mapitio ‘Review’ ya shauri la mchezaji Feisal Salum ‘Fei Toto’ na klabu ya Yanga juu ya sakata la mkataba baina ya pande hizo mbili huku wakili mzoefu, Fatuma Karume akionekana kukabidhiwa mafaili ya kiungo huyo wa Yanga.
Awali Fei Toto alisimamiwa na mawakili Nduruma Majembe na Makubi Kanju lakini leo wameonekana kuongeza nguvu kwa kumuongeza Fatuma kwenye jopo hilo na wakili huyo ndiye ametinga makao makuu ya TFF, Karume akiambatana na kiungo huyo.
Wakiwa katika gari nyeusi aina ya Alphard yenye ‘tinted’ Fei Toto na Fatuma waliwasili katika ofisi hizo saa 2:57 asubuhi na dakika 10 baadaye alifika mama mzazi wa mchezaji huyo akiwa kwenye gari aina ya Prado.
Baada ya mama huyo kufika waliongozana kwa pamoja wakaingia kwenye moja ya vyumba vya ofisi za TFF, kisha wakatoka na kujifungia kwenye gari wakionekana kuwa na kikao.
Saa 9:45, iliingia gari nyingine aina ya Harrier iliyokuwa nawakili Nduruma ambaye alimsimamia Fei Toto tangu mwanzo na moja kwa moja akashuka na kuingia kwenye Alphard waliyokuwa wamekaa kina Feisal.
Ikumbukwe Yanga ilipeleka shauri kwenye kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) ikimtaka Feisal kutoa maelezo kwanini ameondoka ndani ya kikosi hicho na kuandika barua ya kuaga akiichapisha katika ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Desemba 24,2022, bila mazungumzo ya pande zote mbili.
Baada ya hapo shauri hilo kwa mara ya kwanza lilisikilizwa Ijumaa ya Januari 6, mwaka huu na TFF ilitoa barua iliyoeleza Feisal bado ni mchezaji halali wa Yanga kimkataba na kutoa nafasi ya upande wa Feisal kuomba mapitio 'Review' ya shauri hilo kama hawataridhika na maamuzi yaliyotolewa.
Hata hivyo, upande wa Feisal kupita kwa mawakili wake hawakukubaliana na majibu ya TFF na kuomba mapitio ambayo hatimaye yatasikilizwa leo.
Kabla ya leo, awali mapitio hayo yalipangwa kusikilizwa Februari 27, lakini ikasogezwa mbele hadi leo Machi 2, 2023.