Simba yaichapa Mtibwa Ndemla akila umeme

Thursday June 23 2022
full pic
By Ramadhan Elias

SIMBA imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliomalizika uwanja wa Benjamin Mkapa.

Pamoja na Mtibwa kupoteza mchezo, imeondoka uwanjani hapo na pigo lingine baada ya kiungo wake Said Ndemla kuoneshwa kadi nyekundu iliyotokana na kumchezea madhambi Sadio Kanoute wa Simba.

Katika mchezo huo, kipindi cha kwanza kilimalizika Simba ikiwa kifua mbele kwa mabao 2-0, yaliyofungwa na Pape Sakho dakika ya 17 na kipa Shaban Kado kujifunga dakika ya 44.

Kipindi cha pili kilirejea kwa timu zote kuendelea kutafuta mabao Simba ikitaka kuongeza huku mtibwa ikipambana kupata bao la kwanza na la kuongoza lakini hadi kufika dakika ya 75 ubao wa matokeo uliendelea kusomeka 2-0.

Katika muda huo, timu zote mbili zilifanya mabadiliko, matatu kwa Mtibwa wakiingia Deo Kanda, Ibrahim Hilka na Stive Nzigamasabo huku Simba ikifanya mawili ikiwatoa Kibu Denis na Pape Sakho ambao nafasi zao zilichukuliwa na Yusuph Mhilu na Taddeo Lwanga.


Advertisement


Kadri dakika zilivyozidi kwenda, kasi ya Mtibwa langoni kwa Simba ilizidi kuongezeka na kudhibitiwa na mabeki wa Simba wakiongozwa na Pascal Wawa anayeagwa kikosini hapo baada ya kucheza kwa misimu minne mtawaliwa.

Simba nayo kupitia kwa Banda, Mhilu na Meddie Kagere ilifanya mashambulizi ambayo hayakuzaa mabao.

Hadi dakika 90 zinamalizika, ubao wa mabao ulikuwa ukisomeka Simba 2-0 Mtibwa Sugar.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha alama 60 na kusalia nafasi ya pili kwenye msimamo huku Mtibwa ikibaki na pointi 31 nafasi ya 12 na timu zote zikiwa zimesaliwa na mechi mbili tu.

Advertisement