Simba wafuzu hatua ya makundi kibabe

MCHEZO wa Klabu Bingwa Afrika kati ya Simba na FC Platinum umemalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa bao 4-0, mabao yaliyofungwa na Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, John Bocco na Clatous Chama.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kuendelea walipoishia kwani waliingia kwa kushambulia kama ilivyokuwa kipindi cha kwanza na dakika ya 50, Luis Miquisone alipiga mkwaju wa faulo uliogonga mwamba wa juu baada ya kuangushwa na beki wa Platinum nje kidogo ya boksi la 18.

FC Platinum nao walionekana kuchachamaa kwa kwani katikati ya dakika 50 hadi 55 waliweza kupata kona mbili ambazo hazikuleta madhara yeyote kwenye lango la Simba, pia dakika ya 57 mshambuliaji mmoja wa Platinum alikosa bao la wazi akiwa amebaki yeye na kipa na kupiga mpira uliotoka nje.
Dakika ya 60 Simba walifanya mabadiliko kwa kumtoa Said Ndemla na nafasi yake kuchukuliwa na Ibrahim Amme na dakika ya 61 Simba wakapata bao la pili kupitia kwa beki wao wa kulia Shomari Kapombe.
Baada ya bao hilo la pili kwa Simba mchezo mchezo kwa ujumla ulifunguka na timu zote mbili kuanza kucheza kws kutafuta bao japo Plutinum walionekana kuliandama mara kwa mara goli la Simba.

Dakika ya 75 Simba walifanya mabadiliko mengine kwa kwa kumtoa Straika Chriss Mugalu na nafasi yake kuchukuliwa na Meddie Kagere.
Dakika 85 John Bocco aliingia kwa upande wa Simba kuchukua nafasi ya Meddie Kagere aliyeumia dakika chache baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Chriss Mugalu.
Dakika ya 90 John Bocco aliiandikia Simba bao la tatu na la mwisho kwa mchezo huo baada ya kumalizia pasi safi ya Larry Bwalya.
Dakika ya 90 (Nyongeza) Simba walipata bao la nne kupitia Chama kwa mkwaju wa Penalti baada ya Chama huyo huyo kuangushwa ndani ya boksi la 18 na mlinzi mmoja wa Platinum.

Ushindi huo wa bao 4-0 unawafanya Simba kufuzu hatua ya Makundi ya michuano hiyo kwa jumla ya bao 4-1, kutokana na mchezo wa kwanza uliochezwa Zimbabwe FC Platinum kushinda kwa bao moja pekee.
Yaliyojiri
Wakati straika wa Simba, Meddie Kagere akiwa anagangwa chini akiwa amepigwa kipepsi na mchezaji wa upinzani baada ya kuingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Chris Mugalu.
Wachezaji wa FC Platnum ambao walikuwa wanafanya mazoezi ya kupasha misuri, walikuwa wanapiga mpira katika lango alilokaa kipa wa Simba, Aishi Manula.
Ukiachana na vituko vya wachezaji wa Platnum, mashabiki wa Simba bila kujali kukamatwa na askari walikuwa wanaingia uwanjani kukumbatia wachezaji wao.
Chama ndiye aliyeonekana kukumbatiwa zaidi, akifuatwa na nahodha wao John Bocco ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Kagere aliyeshindwa kuendelea baada ya kupigwa kipepsi.