Ally Salim kumrithi Beno Namungo

Muktasari:
- Chanzo cha kuaminika kutoka Namungo kimeliambia Mwanaspoti kuwa, mazungumzo kati ya timu hiyo na uongozi wa Simba yanaendelea vizuri huku kikibainisha nyota huyo bado ana mkataba alipo.
BAADA ya kumalizana na Beno Kakolanya waliyemsajili kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea Singida Black Stars uongozi wa Namungo upo katika mazungumzo na kipa wa Simba, Ally Salim.
Chanzo cha kuaminika kutoka Namungo kimeliambia Mwanaspoti kuwa, mazungumzo kati ya timu hiyo na uongozi wa Simba yanaendelea vizuri huku kikibainisha nyota huyo bado ana mkataba alipo.
“Mkataba wa Salim na Simba utafikia tamati mwaka 2027 na kilichopo ni mazungumzo na waajiri wake licha ya kwamba hayupo kwenye mpango wa timu hiyo msimu ujao hivyo tunatarajia lolote l;inaweza kutokea akaweza kuwa sehemu ya kikosi chetu,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Tunamuhitaji na tunatambua uwezo wake tunaamini ataweza kutusaidia kutokana na uzoefu alionao licha ya kutokupata nafasi ya kucheza mara kwa mara lakini tunaamini akipata nafasi atafanya kitu kikubwa na kizuri.”
Wakati mtoa taarifa huyo akifunguka hayo Mwanaspoti linafahamu kuwa Salim ni sehemu ya wachezaji watakaoachwa Simba katika dirisha hili lililofunguliwa kwa msimu ujao, huku kipa wa JKT Tanzania Yakubu Suleiman akitajwa kuwa mbadala sahihi.
Simba msimu ujao inatarajia kuwa na mabadiliko makubwa ndani ya kikosi ikielezwa kuwa mbali na Salim ambaye alikuwa kipa namba mbili kikosini, inaelezwa kuwa mazungumzo ya kumwongeza mkataba mpya Moussa Camara yamesitishwa.
Salim alijiunga na Simba akitokea timu ya vijana na tangu apandishwe timu ya wakubwa akitokea Simba B mwaka 2018-2024, timu hiyo imechukua mataji manne ya Ligi Kuu Bara, msimu wa 2017/18, 2018/19, 2019/20 na 2020/21.