Ibenge aanza mambo ya msimu ujao Azam

Muktasari:
- Kiongozi mmoja kutoka timu hiyo, alieleza ujio wa Ibenge ni kwa ajili ya kujadiliana na viongozi kuhusiana na maandalizi ya msimu mpya kama maboresho ya kikosini kwa wachezaji wapya na watakaochwa.
KOCHA Florent Ibenge anayetajwa kuja kuinoa Azam FC msimu ujao, imedaiwa tayari yupo nchini tangu juzi Alhamisi na amekutana na mabosi wa klabu hiyo kuanza rasmi kazi kwa kuweka mipango sawa kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2025/26 na michuano ya kimataifa.
Kiongozi mmoja kutoka timu hiyo, alieleza ujio wa Ibenge ni kwa ajili ya kujadiliana na viongozi kuhusiana na maandalizi ya msimu mpya kama maboresho ya kikosini kwa wachezaji wapya na watakaochwa.
“Ibenge tunamtarajia kuingia nchini leo (jana), ili kuanza mipango kwa ajili ya msimu ujao tutamsikiliza mapendekezo yake ya wapi anataka timu ikaweke kambi kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao,” alisema kiongozi huyo na kuongeza;
“Kuna ripoti aliyoacha kocha Rachid Taoussi atakabidhiwa Ibenge kuitumia kwa ajili ya usajili, kitu kizuri zaidi kocha huyo anaifuatilia Ligi ya Tanzania na anawafahamu wachezaji wengi, kitu ambacho kitamrahisishia kupata machaguo anayoyataka.”
Ibenge tayari alishaaga katika klabu Al Hilal ya Sudan aliyokuwa anaifundisha msimu uliopita, hivyo Azam inasubiri kumtangaza kuanza majukumu yake mapya, kabla ya timu hiyo Simba na Yanga miaka ya nyuma zilijaribu kuhitaji huduma yake lakini zilijikuta zinagonga mwamba.
WASIFU WAKE
Ibenge alianza kazi ya ukocha nchini Ufaransa, alizinoa timu za ES Wasquehal na SC Douai, mwaka 2012 alipata fursa ya kuwa kocha wa klabu ya Shanghai Shenhua nchini China alikokaa kwa kipindi kifupi, kisha 2014 alirudi Afrika kuifundisha AS Vita Club ya DRC.
Mwaka huohuo, Ibenge aliteuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya DR Congo (Leopards) akiipa ubingwa wa mashindano ya African Nations Championship (CHAN) mwaka 2016. Hata hivyo, mwaka 2017 alijiuzulu kuwa kocha wa taifa na 2019 akarudi tena Vita.
Mwaka 2021, Ibenge alienda Morocco kujiunga RS Berkane kama kocha mkuu, 2022 alikwenda Sudan kuifundisha Al-Hilal akiisaidia timu hiyo kutwaa Kombe la Sudan kwa ushindi wa penalti dhidi ya Al Ahli Khartoum.
Lakini kazi yake ilikatizwa na kuzuka kwa vita nchini Sudan mwaka 2023, hali iliyoilazimisha timu hiyo kuhamia Cairo, Misri kuweka kambi, mwezi Aprili 2023 aliondoka Sudan na familia yake na kuelekea Ufaransa kupitia Djibouti kwa ajili ya usalama wao.