Nyota wazawa Azam washushwa Presha

WAKATI  Ligi Kuu Bara ikiwa ukingoni, baadhi ya wachezaji wazawa wakiwemo wa Azam wapo matumbo joto kutokana na mikataba yao kuelekea ukingoni na wengine wakihofia kutemwa na kupisha majembe mapya kuingia.

Katika kuzingatia hilo, Mwanaspoti lilizungumza na kocha msaidizi wa Azam, Vivier Bahati kujua hatima ya baadhi ya nyota wazawa kuelekea msimu ujao ambapo alifafanua kuwa huenda wengi wao wakasalia kikosini hapo.

"Tunathamini kila mchezaji, lakini pia ili kuhakikisha tunazidi kuwa bora zaidi lazima tufanye usajili na kuachana na baadhi ya wachezaji. Hadi sasa hatujapanga kuachana na yeyote lakini hata ikiwa hivyo wazawa wengi hawako kwenye mipango ya kuachwa," alisema Vivier na Kuongeza:

"Tumewaongeza mikataba baadhi yao akiwemo Iddi Nado na Ayoub Lyanga na wengine wenye mikataba watabaki. Tunaweza kuwa na wazawa wengi lakini wale wa kigeni sheria inataka wawe 10 tu, hivyo lazma baadhi waondoke ili nafasi ya usajili wa wengine ipatikane lakini kwa wazawa huenda wakabaki wote," alisema Vivier.

Tetesi zinasema huenda kipa David Kisu akawa miongoni mwa wachezaji wachache watakaoachana na Azam msimu huu baada ya kushindwa kuwa na muendelezo mzuri wa kiwango chake.