Mwanaspoti tuko Live Kigoma

TAARIFA ikufikie wewe msomaji wa Mwanaspoti kwamba tutakuwa ‘live’ kuanzia leo kutoka mjini Kigoma kukuletea kila kitu mpaka mechi ya Simba na Yanga itakapomalizika.

Utapata kila kitu kinachoendelea ndani na nje ya kambi, mitaani na kila sehemu kupitia kwenye Gazeti la Mwanaspoti na mitandao yetu ya kijamii instagram, tovuti, Twitter na Mwananchi Digital.

Mwiliweee! Ndiyo salamu kubwa mkoani Kigoma ambapo wikiendi hii mkoa huo unaenda kusimama na kusisimka kwa kushuhudia fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Waha ndio kabila kubwa mkoani hapa na Mwiliwe ndiyo salamu yao kubwa licha ya kwamba asubuhi husalimiana ‘Mwakeye’ na ukisalimiwa Mwiliwe unatakiwa kujibu hivyo hivyo, Mwiliwe.

Kigoma inaenda kuandika rekodi ya kuhodhi fainali ya Kombe la ASFC inayohusisha timu zenye mashabiki wengi zaidi Tanzania, Simba na Yanga, mchezo utakaopigwa Jumapili ndani ya Uwanja wa Lake Tanganyika.

Chama cha Soka mkoani Kigoma (KFA) kupitia kwa katibu mkuu, Omary Gindi amefunguka kuwa: “Maandalizi yamekamilika, tulifanya kikao na Serikali ya Mkoa wa Kigoma ikiongozwa na Mkuu wa mkoa, Thobias Andengenye kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali kuhusu mchezo huo mkubwa hapa mkoani kwetu, ikiwemo suala la ulinzi ambalo mkuu wa mkoa ametuhakikishia ulinzi wa kutosha kuanzia nje na ndani ya uwanja,” alisema Gindi.

“Tumepata ugeni mkubwa kutoka kwa maofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambao wamekuja hapa kwa ajili ya kuangalia maandalizi mazima ya uwanja na kujiridhisha kwa hatua kubwa tulizofikia na kilichobaki ni siku ifike, mechi ichezwe, watu wapate burudani.”

Pamoja na watu wa Kigoma kuzisubiri kwa hamu timu zao, Simba na Yanga kuwasili mkoani humo kwa ajili ya mechi hiyo inayotarajiwa kuwa kali, taarifa kutoka mkoani humo zinaeleza kuwa wapenzi wa soka na mashabiki wa timu hizo kutoka sehemu mbalimbali nchini wameanza kuwasili kwa wingi tayari kushuhudia fainali hiyo ya kibabe.

Makocha wa timu zote mbili, Didier Gomes wa Simba na Nasreddine Nabi wa Yanga wametambiana kujiandaa kushinda mechi hiyo na kubeba ubingwa huo.

Gomes amsema: “ Ni mechi ya heshima ambayo tunajipanga kwenda kushinda na kuchukua kombe ili tufunge msimu vizuri na kuwapa furaha mashabiki wetu kabla hatujaanza msimu mpya.”

Naye Nabi amesema: “Kila mpenzi wa Yanga analitaka kombe hili, hata sisi kama timu tunalitaka pia, hivyo tunajiaanda kuhakikisha tunabeba.”