Morrison: Niachieni mimi hao Yanga

DAKIKA 45 alizotumia Bernard Morrison kukiwasha kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa wakati chama lake la Simba likiwanyoosha Kagera Sugar, limefanya winga huyo Mghana kuwa gumzo kuelekea kwenye Kariakoo Derby, huku mwenyewe akisema anataka aachiwe awashukie.

Morrison aliingizwa kipindi cha pili na Kocha Didier Gomes kwenye mchezo huo wa 16 Bora ya michuano ya ASFC na kufunga bao la kusawazisha kabla ya kutoa pande tamu kwa Meddie Kagere aliyefunga bao la ushindi dhidi ya Kagera na kuivusha Simba hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Soka alilopiga Mghana huyo lilikuwa kama salamu kwa Yanga ambao msimu uliopita aliichezea na ndiye aliyefunga bao pekee lililowapa ushindi Vijana wa Jangwani.

Katika mchezo wa juzi, winga huyo aliingia uwanjani kuchukua nafasi ya kiungo Taddeo Lwanga wakati Simba ikiwa nyuma kwa bao 1-0 lililofungwa kwa kichwa na Erick Mwaijage na kubadilisha kabisa kasi ya mchezo akifunga bao kumalizia krosi ya Shomary Kapombe kabla ya kumpasia Kagere aliyekwamisha bao la ushindi.

Ubora wa Morrison kwenye mechi hiyo uliwafanya wadau na mashabiki wengi wa soka nchini kudai ni salamu tosha zilizotumwa na winga huyo kwa Yanga kabla ya kuvaana Jumamosi, huku mwenyewe akisema kwa kifupi yeye ni Simba na yupo Simba hivyo anatakiwa aachiwe mwenyewe.

“Kwa sasa sitaki kuzungumza sana, tunachohitaji ni kushinda ili tufikie malengo na kuwafurahisha masha-biki wetu. Kuhusu mechi na Yanga haina haja ya mimi kuizungumzia kwani naichezea Simba na mimi mwenyewe ni Simba, hivyo naamini kila mtu anajua kazi ya Simba,” alisema Morrison.

Licha ya Morrison kushindwa kufunguka zaidi juu ya derby, lakini baadhi ya wadau akiwamo beki wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Boniface Pawasa alisema; “Morrison ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa lakini anahitaji kocha mbunifu zaidi ili kumtumia. Nimependa namna Gomes anavyomtumia, mara nyingi amekuwa akimpa nafasi kutokea benchi na hubadili mchezo hivyo kama atamuamini kwenye mechi dhidi ya Yanga anaweza akawathibitishia kuwa anafanya anachokielewa.”

Naye kiungo fundi wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka, Ally Mayay alisema; “Kwa tabia ya Morrison na mazingira ya mechi ya mahasimu kama hiyo ya Mei 8 ni dhahiri ni mchezaji muhimu sana na ataisaidia timu kwa vitu tofauti. Akipewa nafasi atahitaji kuonyesha ubora, pia atahitaji kufanya jambo kubwa kwani tayari anaujua utamaduni wa soka letu.

“Aidha, kiuchezaji, Morrison muda wote anataka kushambulia na huwa hatari zaidi kwa wapinzani, hivyo hiyo inaweza kuwa faida kwa Simba na kuwapa kazi ya ziada Yanga katika mchezo huo,” aliongeza Mayay.

Kwa upande wa upande wa Kocha Didier Gomes alikiri Morrison ni jembe na mtu wa kuamua matokeo wakati wowote na kwa kiwango alichoonyesha dhidi ya Kagera kimemfurahisha na yupo kwenye mipango yake kwa mechi zijazo.