Kibu ataka mabao zaidi Simba

Thursday June 23 2022
kibu pic
By Ramadhan Elias

BAADA ya kutupia bao lake la nane msimu huu wa Ligi Kuu Bara na kuwa kinara wa mabao ndani ya Simba, nyota wa timu hiyo, Kibu Denis ameeleza kutaka mabao zaidi kabla ya msimu kumalizika.

Kibu alijiunga Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Mbeya City na tangu amejiunga na Wekundu wa Msimbazi amekuwa na muendelezo bora wa kiwango chake na sasa anataka kufunga mabao 10 au zaidi.

“Kuna muda unafunga na muda mwingine inatokea unakosa. Nashukuru kupata nafasi na kufunga mabao.”

“Malengo ni kuifanya Simba ifanye vizuri na kupata ushindi mechi zilizobaki na binafsi natamani kuendelea kufunga na ikiwezekana msimu huu nimalize na mabao kuanzia 10 na kuendelea,” alisema.

Kaimu kocha mkuu wa Simba, Seleman Matola alimuelezea Kibu kuwa ni mchezaji anayejituma zaidi na muda mwingi hutumia kujifunza na kukosoa makosa yake ili awe bora zaidi.

“Ni mchezaji mzuri, anapambana sana kuhakikisha timu inatimiza malengo pia malengo yake binafsi, tutaendelea kumtumia,” alisema Matola. Kibu ndiye anaongoza kwa ufungaji Simba akifuatiwa na Meddie Kagere mwenye mabao saba huku George Mpole (Geita Gold) na Fiston Mayele (Yanga) wakiongoza vita ya kuwania kiatu cha mfungaji bora kwa msimu huu kila mmoja ana mabao 16.

Advertisement
Advertisement