Kagere aongeza nguvu ushambuliaji Simba

Thursday October 14 2021
kagere pic
By Oliver Albert
By Ramadhan Elias

ENEO la ushambuliaji la Simba limeendelea kupata nguvu baada ya nyota wake Meddie Kagere kurejea kikosini hapo akitokea kwenye timu yake ya taifa ya Rwanda ‘Amavubi’.

Kagere ambaye aliifungia bao la kwanza kwenye Ligi Kuu msimu huu likiwa ni bao pekee na la ushindi dhidi ya Dodoma Jiji, ameonekana katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika katika Uwanja wa Boko Beach Veteran, Dar es Salaam.

Licha ya kwamba hakufanya mazoezi na Simba kwa zaidi ya siku tano zilizopita wakati akuwa Amavubi, nyota huyo leo ameingia moja kwa moja kwenye mazoezi ya jumla na wachezaji wote na kuonesha ubora.

Uwepo wa Kagere umeifanya Simba kuwa na jumla ya washambuliaji wa kati watatu katika mazoezi ya leo akiungana na nahodha wa timu hiyo John Bocco sambamba na Kibu Denis.

Baada ya Kagere kuwasili, wachezaji waliokuwa katika timu zao za taifa ambao hawajawasili wamebaki wawili tu, Peter Banda na Dancun Nyoni ambao walikuwa katika timu ya taifa ya Malawi na muda wowote kuanzia leo waajiunga na kikosi hicho.

Simba inajiandaa na mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Africa kwa msimu huu dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana uliopangwa kuchezwa Oktoba 17 kwenye Uwanja wa taifa hilo na kesho Oktoba 15 kikosi hicho kitapaa kwa ndege maalumu kuelekea Botswana kwaajili ya mechi hiyo.

Advertisement
Advertisement