Hersi: Manji akija mmeisha

HERSI Said amewaambia Yanga kwamba kama kweli Yusuf Manji akirejea Jangwani kikosi hicho kitatisha. Hersi ambaye kitaaluma ni injinia akiiwakilisha GSM ambao ni miongoni mwa wadhamini wa Yanga, amewahakikishia wanachama na mashabiki kwamba wako tayari kufanya kazi na Manji.

Manji ambaye ni Mwenyekiti wa zamani wa Yanga na kipenzi cha mashabiki, alirejea Jijini Dar es Salaam wiki hii baada ya kukaa ughaibuni miaka kadhaa.

Mmoja wa watu wa karibu wa Manji ambaye aliwahi kununua mastaa kibao walioipa kiburi Yanga, amelidokeza Mwanaspoti kwamba tajiri huyo amewaambia akishaweka ishu zake sawa ataangalia namna nzuri ya kuwekeza Jangwani.

Hersi alisema; “Ujio wa Manji ni kama baraka kwetu, tumekuwa tukiita wadau wengi kuja kuiunga mkono GSM kwenye kuendesha timu yetu, gharama ni kubwa, tunalipa kambi na vitu vingine vingi ambavyo ni vinataka pesa.

“Manji ni mdau wa Yanga na anaipenda timu hii, akija kwa namna moja ama nyingine anaweza kufanya timu hii ikawa bora zaidi Afrika na kuwa tishio,” alisema Hersi.

Hersi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya klabu hiyo, aliongeza kuwa; “Msimu huu tulifanya usajili mkubwa wa wachezaji wenye ubora na wamekuja Yanga na kuongeza ubora wao, kila mmoja amefanya vyema na kwa maendeleo makubwa kwa timu na kwa wao binafsi.

“Ukiangalia wachezaji kama Yassin Mustafa na Tonombe Mukoko wameitwa kwa mara ya kwanza kwenye timu zao za taifa wakitokea Yanga, pia Yacouba Sogne ameitwa timu yake ya taifa msimu huu akitokea Yanga jambo ambalo hakufanya hivyo akiwa Asante Kotoko hivyo hiyo inaonyesha ni namna gani Yanga ni timu kubwa,” alisema Hersi.

“Nakumbuka tuliingia kwenye vita na majirani zetu Simba juu ya usajili wa Bakari Mwamnyeto lakini tukashinda, kiufupi ni kwamba hakuna ambaye angetuzuia na atatuzuia kumpata mchezaji tunayemtaka,” alisema.

Pia Hersi aliwazungumzia wachezaji ambao wapo Yanga lakini wameshindwa kuonyesha makali yao na wengi wameishia kukaa benchi tu.

“Jambo la kusajili mchezaji na asing’ae ni la kawaida, lakini kwa asilimia kubwa wachezaji tuliowasajili msimu huu wamefanya vizuri na ambao wameshindwa kuonyesha ubora tutaachana nao kwa mapendekezo ya benchi la ufundi,” alisema Hersi na kuongeza;

“Tufanya usajili kwa misingi iliyopo kwa kuanzia kwenye mapendekezo ya kocha, kamati ya ufundi, mwenyekiti na wengine lakini kadri siku zinavyosonga tutahama kuwa kisasa zaidi, pamoja na yote hayo wachezaji tutakaowasajili msimu ujao watakuwa wenye ubora na hadhi ya kucheza Yanga.

“Kazi ya GSM ni kutoa pesa, kama GSM kazi yetu sio kuchagua mchezaji wala kupendekeza ni mchezaji gani anatakiwa kusajiliwa hivyo mkiniona kwenye lile kochi na mchezaji, mimi nakuwa nasimama kama mtoa fedha na sio mtu aliyesajili,” alisema Hersi ambaye mapema msimu huu alikaririwa akiwaambia mashabiki wa Yanga kama timu yao isipochukua ubingwa aulizwe yeye.

“Kuna maendeleo makubwa sana ambayo tumeyafanya kwa timu yetu, kati ya hayo ni suala la uchumi. Miaka ya nyuma timu ilikuwa inapata taabu hata kulipa mishahara lakini leo wachezaji wanapata maslahi yao mapema na wanaridhika,” alisema Hersi na kuongeza;

“Jambo jingine ni la kiuongozi, tumefanya vizuri tumeleta wataalamu tofauti wenye ubora wao akiwemo Senzo Mazingisa, hakuna shaka hadi sasa jezi yetu ndiyo bora na ya kuvutia zaidi Afrika Mashariki.”