Biashara yajificha kuisubiri Simba

Monday September 27 2021
biashara pic
By Ramadhan Elias

KOCHA mkuu wa Biashara United Patrick Odhiambo tayari amemaliza hesabu za kiufundi kuelekea kesho kwenye mechi ya kwanza ya ligi kwa msimu wa 2021/2022 dhidi ya Simba na sasa timu hiyo imejificha kimya kimya mjini Musoma.

Mwanaspoti ambalo litakua laivu kuanzia leo jioni mjini Musoma linataarifa kuwa wachezaji na benchi la ufundi la Biashara wamefichwa katika moja ya hoteli za mjini humo na hakuna mtu anaruhusiwa kwenda zaidi ya viongozi pekee.

Licha ya kushindwa kutaja Hoteli iliyopo timu hiyo, mmoja wa Vigogo wa wanajeshi hao wa mpakani ameeleza kuwa tayari wamefunga hesabu na sasa wanasubiri muda wa mechi ufike wakatafute alama tatu muhimu.

“Tumemaliza kila kitu na sasa tupo sehemu ya maficho tunasubiri kesho ifike tukaanze ligi kwa kishindo.

Kocha na wachezaji wamemaliza programu zote na leo jioni hatufanyi mazoezi, tutawaachia Simba Uwanja.” amesema Kigogo huyo.

Mechi hiyo itapigwa kesho saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Karume Musoma na inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na timu hizo kumaliza katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa msimu uliopita, Simba ikiwa Bingwa na Biashara ikamaliza nafasi ya nne.

Advertisement

Kwa mara ya mwisho timu hizo kukutana kwenye mechi ya ligi ilikua Februari 18, 2021 kwenye Uwanja huo huo wa Karume, Musoma na Simba kushinda bao 1-0, lililofungwa na Bernard Morrison.

Advertisement