Biashara, Simba ngoma ngumu dakika 45

DAKIKA 45 za kipindi cha kwanza za mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Biashara United na Simba zimemalizika kwa suluhu (0-0) kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma.

Mchezo ulianza kwa timu zote mbili kushambuliana kwa presha kubwa na timu zote mbili kuonekana kuwa imara kila idara.

Namna dakika zilivyozidi kwenda Simba ilianza kucheza mipira mirefu kutoka kati kwa Hennoc Inonga na Erasto Nyoni kwenda kwa Meddie Kagere na John Bocco ambao walidhibitiwa na mabeki wa Biashara wakiongozwa na Abdul Majid Mangalo.

Dakika ya 20, Simba kidogo wapate bao baada ya Rally Bwalya kupiga pasi ya juu iliyomkuta Kagere kwenye boksi la 18 la Biashara na kupiga kichwa mpira ukaenda nje kidogo ya lango la Biashara.

Dakika ya 30 hadi ya 32 Biashara walimiliki mpira kwa kupigiana pasi fupi fupi zisizopungua tano kabla ya Simba kuchukua mpira na kufanya shambulizi ambalo Kagere alipiga Kiki ya kawaida iliyoenda nje ya goli.

Denis Nkane dakika ya 33 kidogo aipatie bao la kuongoza Biashara kwa kupaisha mpira uliomkuta ndani ya boksi la 18 la Simba akiwa amebaki yeye na kipa, Manula tu.

Presha iliendelea kuwa kubwa kwa timu zote mbili na kuendelea kucheza mpira wa kushambulia kwa kushitukizana licha ya kwamba mara nyingi Simba ndiyo ilionekana ikishambulia lango la Biashara.

Kagere tena dakika ya 37 akiwa ndani ya boksi la 18 la Biashara alipiga kichwa akimalizia krosi ya Bwalya lakini mpira ulipaa juy ya goli.

Dakika ya 40 Biashara kidogo wapate bao kupitia kwa Nkane aliyeingia ndani ya boksi la 18 la Simba na kubaki na kipa akapiga mpira uliopanguliwa na Manula kisha kukkuta Atupele Green na Kuchelewa kuupiga na Manula kuudaka.

Kipa wa Biashara, James Ssetuba alionekana kuwa shujaa wa dakika 46 za kipindi cha kwanza kwa kuokoa mashuti na kuzuia nafasi nyingi zilizotengenezwa na Simba.

Hadi dakika 45, za kipindi cha kwanza zinamalizika Biashara 0-0 Simba.