Simba yaleta kocha Mreno

MUDA wowote kuanzia wakati huu mabosi wa Simba wapo kwenye hatua za mwisho kumtangaza kocha mkuu mpya ambaye mchakato wake wa kumpata umekamilika na anasubiri tiketi ya ndege ili kutua nchini Jumatatu.

Mwanaspoti asubuhi ya jana Alhamisi lilimshuhudia kiongozi mmoja wa juu akiwa na harakati za kufuatilia visa, tiketi ya ndege pamoja na kibali cha kazi ili baada ya kocha huyo kufika kila kitu kiwe sawa.

Kiongozi huyo akiwa kwenye mchakato wa mambo hayo Mwanaspoti limepata uhakika kocha mpya wa Simba atakuwa ni Mreno na muda wowote kuanzia sasa atawasili nchini na mara baada ya kutambulishwa atakwenda moja kwa moja kambini kujiunga na wachezaji kwa ajili ya kuanza kazi.

Kocha huyo haikuwa rahisi kupata jina lake kutokana na usiri mkubwa wa mabosi wa Simba waliyouweka licha ya Mwanaspoti kufahamu muda wowote atawasili nchini na ataanza kazi ya kukinoa kikosi cha Simba.

Mwanaspoti halikuishia hapo limejiridhisha kocha huyo mpya wa Simba, Mreno hatakuja kwenye kikosi cha Simba peke yake, bali atatua na wasaidizi wake wawili watakaokwenda kufanya kazi kwenye nafasi mbili tofauti.

Msaidizi wake wa kwanza atakuwa kocha wa viungo na Mwanaspoti linafahamu mtaalamu huyo atakuwa ni Msauzi Afrika, Kelvin Mandla, na ametokea nchini humo kwani kila kitu kimemalizika hadi masuala ya kimaslahi.

Kocha huyo mpya wa viungo Msauzi amependekezwa na mtaalamu wa kuchua misuli ndani ya Simba, Fareed Cassim ambaye naye ni raia wa nchi hiyo aliwahakikishia mabosi zake kwamba anaufahamu uwezo wake wa kufanya kazi.

Baada ya mabosi wa Simba kupitia wasifu wa kocha huyo mpya wa viungo walilizika naye na kwenye mazungumzo yao kila kitu kimeenda sawa na muda wowote kuanzia sasa anatua nchini kwa ajili ya kuanza kazi.

Baada ya mabosi wa Simba kukubaliana na kocha wa viungo tafsiri yake dili la kocha wa viungo kutoka Timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ Michael Igendia limekufa rasmi na sababu kubwa ikielezwa ni masuala ya kimaslahi licha ya kutua nchini.

Msaidizi mwingine wa Kocha Mreno atakayekuja naye ni mtaalamu wa kuchambua mechi kupitia video (Video Analyst), ili kuliongezea nguvu benchi la ufundi. Katika majadiliano mabosi wa Simba walimueleza kocha wao mpya Mreno kuwa video analyst yupo ndani ya kikosi hicho, Mzimbabwe Culvin Mavunga lakini aliwajibu watafanya kazi wote kwa pamoja na atawapa majuku.

Mreno huyo aliwambia mabosi wake Mavunga kwa kuwa ni mwenyeji atakuwa anafanya kazi ya kuwasoma wapinzani wake huyo ambaye atakuja naye atafanya kazi ya kuisoma timu yake kabla na baada ya mchezo.

Baada ya Mreno huyo kutambulishwa atakuwa mkuu wa benchi la ufundi chini yake kutakuwa na wasaidizi wawili, Juma Mgunda na Selemani Matola ambaye Novemba 21 atakwenda kwenye kozi ya ukocha wa Diploma ‘A’ ya Shirikisho la soka Afrika na atakuwa huko kwa wiki mbili.

Kukosekana kwa Matola ndani ya Simba kwa muda huo linaweza lisiwe tatizo kwani Mreno atabaki na Mgunda pamoja na wasaidizi wengine akiwemo kocha mpya wa makipa, Mmorocco Chlouha Zakaria aliyeanza kazi kwenye mazoezi ya jana Alhamisi jioni.

Alipotafutwa Mgunda alisema litakuwa jambo jema uongozi kama utamleta kocha atakayesaidiana naye wakati Matola akiwa masomoni kwani akibaki peke yake atakuwa mpweke na litakuwa si jambo jema kama watakapokuwa wawili wakisaidiana na kushauriana.

“Nitampokea yoyote atakayekuja kufanya kazi hapa. Ni jambo zuri kwetu kwani uongozi unataka kuona timu ikifanya vizuri ndio maana inaboresha na kuongeza nguvu kwenye benchi la ufundi,” alisema Mgunda ambaye aliwahi kuitumikia Coastal Union ya Tanga.