Prime
Dabi ya Juni... Yanga 5 Simba 2

Muktasari:
- Hiyo ni kutokana na ukweli pambano hilo limeshikilia hatma ya ubingwa wa Ligi kwa msimu huu ambapo Simba na Yanga zitakutana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, na timu yoyote itakayoibuka na ushindi itakuwa imetwaa ubingwa.
LICHA ya kwamba keshokutwa kuna mechi za kukamilishia raundi ya 30 ya Ligi Kuu Bara ambako vinara Yanga wataivaa Dodoma Jiji na Simba itapepetana na Kagera Sugar, akili za mashabiki wengi wa soka ziko katika pambano la Dabi ya Kariakoo la Juni 25.
Hiyo ni kutokana na ukweli pambano hilo limeshikilia hatma ya ubingwa wa Ligi kwa msimu huu ambapo Simba na Yanga zitakutana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, na timu yoyote itakayoibuka na ushindi itakuwa imetwaa ubingwa.
Kwa sasa Yanga inaongoza msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 76, moja zaidi na ilizonazo Simba iliyo ya pili kwa alama 75, baada ya kila moja kucheza mechi 28.
Jumapili kwenye Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam, Wekundu wa Msimbazi watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar ambayo tayari imeshashuka daraja, wakati Yanga itakuwa kwenye Uwanja wa New Amaan, Unguja visiwani Zanzibar dhidi ya Dodoma Jiji kabla ya Jumatano kuanzia saa 11:00 jioni kuvaana na Simba katika Dabi, huku rekodi za ndani ya Juni zikiwabeba Wananchi katika mechi tisa zilizopigwa katika mwezi huo ikishinda tano.
Mechi mbili baina ya timu hizo zilipokutana Juni, ziliisha kwa sare sawa na zile ambazo Simba ilishinda katika mwezi huo ni mbili, lakini kwa mechi zilizopigwa ndani ya Jumatano, hakuna mbabe baina ya timu hizo kwani kila moja imeshinda tatu na pambano moja liliisha kwa sare.
Rekodi zinaonyesha pambano lijalo la watani kupambana Juni 25 litakuwa la pili, kwani ziliwahi kukutana katika tarehe kama hiyo mwaka 2000 na Simba kushinda kwa mabao 2-1, hivyo kama kismati kikiendelea kuwa upande wa Wekundu, Jumatano ijayo inaweza kuwa neema ya ubingwa kwao.
TISA ZA JUNI
Kwa mujibu wa kumbukumbu za mechi za Dabi ya Kariakoo zilizopigwa Juni tangu kuasisiwa kwa Ligi ya Bara mwaka 1965, mara ya kwanza kukutana kwa timu hizo ilikuwa Juni 7, 1965 na Yanga ikashinda kwa bao 1-0, japo mechi ilipangwa kurudiwa na Yanga ikagoma kisha Simba kupewa ushindi na kubeba taji la kwanza la michuano hiyo enzi hizo timu hiyo ikifahamika kama Sunderland.
Zilikutana tena Juni 3, 1966 na Yanga kushinda kwa mabao 3-2 kabla ya Juni Mosi, 1968 kukutana tena na Mnyama kufumuliwa mabao 5-0 kikiwa kipigo cha kwanza kikubwa baina ya timu hizo na Juni 4, 1972 zilipokutana hakukuwa na mbabe baada ya timu hizo kufunga bao 1-1.
Juni 18, 1972 Yanga ilipata ushindi wa 1-0 mbele ya Simba, kabla ya Juni 23, 1973 Mnyama kutakata kwa ushindi wa 1-0 na Juni 27, 1987 Yanga iliibuka mbabe kwa bao 1-0 la Edger Fongo na Juni 7, 1998 timu hizo zilishindwa kutambiana kwa sare ya 1-1. Mechi ya mwisho kwa mwezi huo iliyopigwa Juni 25, 2000 Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 yote yakifungwa na Steven Mapunda ‘Garrincha’ dk. 59 na 72, baada ya Idd Moshi kuitanguliza Yanga mapema katika dakika ya nne tu.
HUKU HAKUNA MBABE
Kwa mechi zilizopigwa Jumatano kama hii inayokuja ya Juni 25, Simba na Yanga wala hazichekani baada ya kila moja kushinda michezo mitatu na mmoja kumalizika kwa sare, hii ikiwa na maana timu yoyote itakayojipanga vyema ina nafasi ya kushinda Kwa Mkapa katikati ya wiki na kubeba ubingwa.
Mara ya kwanza timu hizo kukutana Jumatano ilikuwa Okt 9, 1991 Yanga iliposhinda 2-0 na kurudia tena Novemba 13, 1991 ilipoichapa tena Simba, hata hivyo mnyama alizinduka Novemba 2, 1994 alipoibuka na ushindi wa bao 1-0 na kutamba tena Oktoba 4, 1995 aliposhinda 2-1.
Oktoba 23, 1996 zilikutana tena Jumatano na Yanga kushinda kwa bao 1-0 na kukaa tena hadi Oktoba 24, 2007 zilipocheza ndani ya siku hiyo na Simba kushinda pia 1-0 na mechi ya mwisho kuvaana Jumatano ilikuwa ni Oktoba 3, 2012 na timu hizo kutoka sare ya 1-1, Simba ikitangulia kwa bao la mapema la dakika ya nne lililofungwa na Amri Kiemba kabla ya Said Bahanuzi kuichomoea Yanga kwa penalti katika dk65.
Pamoja na rekodi hizo bado makocha wa timu hizo, Miloud Hamdi wa Yanga na Fadlu Davids wa Simba wana kibarua cha kufanya kwa mechi hiyo ya Juni 25, kwani kuchemsha kidogo tu itakuwa na maana ya kukubali kuliacha taji mbele ya mpinzani.
Hamdi alikaririwa kwamba hii ni mechi ngumu na kwa kuwa inaamua bingwa, ni lazima ajipange kwa kutambua Simba haitaenda uwanjani kinyonge, huku Fadlu akisema anamalizana kwanza na mechi ya Jumapili kabla ya kuanza mipango kwa ajili ya Dabi aliyodai ni ya kufa au kupona.
Presha imekuwa kubwa kwa wachezaji wa timu hizo mbili, kwa kutambua timu itakayoangusha pointi Kwa Mkapa inapoteza taji, huku Yanga wakisaka rekodi ya kutwaa taji mara nne mfululizo wakati Simba wanatafuta nafasi ya kutwaa baada ya kulisotea tangu ilipotwaa mara ya mwisho 2020-2021.