MGUNDA: maisha ya DR Congo yalikuwa magumu, lakini nimejifunza

Muktasari:
- Mgunda anasema kwa mwanasoka kuishi nje ya Tanzania kunahitaji nidhamu ya pesa, muda, mazoezi na kujua kilichompeleka timu husika ili kufanikiwa kirahisi vinginevyo ni ngumu kufikia malengo.
INGAWA mshambuliaji Ismail Mgunda hakufanikiwa kucheza kama alivyotarajia katika timu ya AS Vita ya DRC Congo, lakini alidhamiria kukipiga nje ya mipaka ya Tanzania. Hapa anasimulia maisha aliyoyapitia nchini humo na anakiri kupata ukomavu na mtazamo chanya.
Mgunda anasema kwa mwanasoka kuishi nje ya Tanzania kunahitaji nidhamu ya pesa, muda, mazoezi na kujua kilichompeleka timu husika ili kufanikiwa kirahisi vinginevyo ni ngumu kufikia malengo.
“Maisha ya Tanzania kwa mchezaji ni tofauti kabisa na DRC Congo ambako kila kitu unapaswa kujitegemea. Hilo litakulazimisha kutumia pesa kwa nidhamu kubwa ukijua kabisa hakuna mtu nyuma yako,” anasema.

“Nimejifunza hilo baada ya kukaa AS Vita bila mshahara wa miezi mitatu. Pesa ilikata kabisa ikawa ngumu kuishi nchi ya watu bila kitu. Inafikia hatua ya kupiga simu Tanzania ili uweze kuendesha maisha, nikaona siyo kitu kinachonipa taswira nzuri ya maendeleo.
“Ilinibidi nivunje mkataba kwa makubaliano maalumu. Sikulipwa pesa, ili wanipe barua ya kuwa huru msimu ukiisha iwe rahisi kupata timu nyingine, hiyo ndiyo sababu ya kurejea Tanzania.
“Kuna kila sababu ya kuwaheshimu wachezaji wanaocheza nje hata kama wanalipwa kwa wakati, ila wana nidhamu ya hali ya juu ya kujisimamia na kuhakikisha viwango vyao vinabaki kuwa juu muda wote kama Mbwana Samatta, Himid Mao, Simon Msuva na wengineo. Bila kumung’unya maneno wanastahili heshima.”

MAISHA YALIKUWAJE
Akizungumzia maisha nchini humo, anasema: “Japokuwa nilikaa kwa kipindi kifupi kubwa mtandao unaotumika Congo ni wa Facebook, hivyo ni ngumu mchezaji kujulikana na kuonekana anachofanya, ndiyo maana wengi wanaotoka huko kuja kucheza ligi ya Tanzania kama Fiston Mayele, Tuisila Kisinda, Beleke (Jean) umaarufu waliupatia hapa.
“Jambo lingine nilijifunza kuthamini amani na utamaduni wetu Watanzania. Sina maana sehemu niliyokuwepo haikuwa na amani, ila utulivu ni mdogo na ngumu kufikiria maendeleo. Nilijua hilo kupitia stori za wazawa, wengi wao wanawaza kuwekeza nje ya nchi yao.”
Anasema hakupata shida kuzoea mazingira na alikutana na aliyekuwa staa wa Yanga, Mahlatse Makudebela maarufu kama Skudu wakawa washikaji na kurahisisha vitu kwenda kirahisi.
“Nilikuwa na ushikaji na Skudu kabla ya kuja Yanga. Niliwahi kwenda kufanya majaribio Afrika Kusini ambako nilikutana naye, hivyo tangu hapo tukawa tunawasiliana. Hivyo nilipokutana naye Congo tukawa kama ndugu,” anasema.

KIMYA CHAKE
Mgunda anasema ukimya baada ya kutoka DR Congo ulitokana na kujipa muda kujua kipi akizungumze na wakati gani. “Nimejifunza kutozungumza kipindi ambacho nina hisia kali, ziwe za furaha ama huzuni. Unaweza ukaongea vitu vinavyoweza kukugharimu maisha yako yote, maana malengo yangu yalikuwa kufanya vizuri nje, ila hilo halikutimia.”

NJE YA KAZI
Mchezaji huyo anaeleza namna maisha yalivyo nje ya kazi yake uwanjani, akidai siyo rahisi endapo mchezaji hajawekeza na kikubwa alichojifunza anapopata nafasi ya kucheza ni kutumia pesa kwa nidhamu ya hali ya juu.
“Kilichonisaidia nisiyumbe kiuchumi nina biashara zangu za vifaa vya umeme kama tv, simu na vitu vingi mbalimbali, hivyo nimepata nafasi ya kuzisimamia na kuongeza maarifa zaidi jinsi ya kuzifanya na kujua soko linataka kitu gani, nje na hapo ningekuwa na msongo wa mawazo,” anasema Mgunda na kuongeza:
“Kinachonisumbua ni arosto ya kutamani kucheza mechi za ushindani, tofauti na mazoezi nayofanya kujiweka fiti, ili nikipata timu nisianze moja kujiandaa, vinginevyo maisha yangu yanaendelea kama kawaida, siwazi nitaishi vipi.”
Ukiachana na changamoto alizotaja, faida anazopata akiitazama Ligi Kuu akiwa nje ni ufundi na juhudi ya mchezaji mmoja mmoja.
“Naangalia ligi kwa utulivu na kujifunza... vitu vingi ninavyovifanyia kazi katika mazoezi. Nafurahia wanachofanya wachezaji wenzangu ufundi wao na bidiii, naamini nikirejea uwanjani nitakuwa na kitu kipya kilichoongezeka katika kazi zangu,” anasema.
Mbali na hilo anasema angeendelea ku-cheza Ligi Kuu hadi sasa angemaliza na mabao kuanzia 10. ”Japokuwa dili la kwenda AS Vita lilikuja katikati ya msimu ila nikaona ni fursa kucheza soka la nje ili kupata uzoefu mpya .”

KIKOSI CHAKE
Kikosi bora cha Mgunda msimu huu ni kipa Yakoub Ali Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Dickson Job, Abdulzack Hamza, Yusuf Kagoma, Elie Mpanzu Simba, Duke Abuya, Clement Mzize Feisal Salum ‘Fei Toto’, Pacome Zouzoua.
“Kwa upande wa kocha bora wa msimu kwa upande wangu ningemchagua Fadlu Davis alianza na kikosi cha wachezaji wapya akakitengeneza hadi kufika fainali za Kombe la Shirikisho Afrika, naamini angekuwa na kikosi kama cha Yanga kingechukua ubingwa kwa mbinu zake,” anasema.
Anasema nje na kikosi bora na kocha, mchezaji aliyemvutia kwa kiwango anachoonyesha ni Fei Toto “Ni kati ya wachezaji wenye vipaji vikubwa nchini. Binafsi kwa msimu huu ningepewa nafasi ya kuchagua MVP ningemtaja yeye. Kacheza mechi nyingi na amehusika katika mabao mengi pia ana mwendelezo wa kufanya vizuri, ndiyo maana timu zinashindana kupata saini yake.”