Prime
Ahoua, Ateba katika vita mpya

Muktasari:
- Yanga inaongoza msimamo kwa sasa ikiwa na pointi 76, moja zaidi na ilizonazo Simba yenye 75 kila moja ikicheza mechi 28 ikiwa na maana mkononi zina michezo miwili ikiwamo baina yao wa Dabi ya Kariakoo utakaopigwa Juni 25, utakaoamua bingwa wa msimu huu.
LIGI Kuu Bara imesaliwa na mechi tisa tu kabla ya kufungwa kwa msimu wa 2024-25, huku Simba na Yanga zikichuana kileleni kuwania ubingwa, lakini kuna vita nyingine mpya imeibuka inayohusisha wachezaji wa timu moja wenyewe kwa wenyewe.
Yanga inaongoza msimamo kwa sasa ikiwa na pointi 76, moja zaidi na ilizonazo Simba yenye 75 kila moja ikicheza mechi 28 ikiwa na maana mkononi zina michezo miwili ikiwamo baina yao wa Dabi ya Kariakoo utakaopigwa Juni 25, utakaoamua bingwa wa msimu huu.
Hata hivyo, wakati klabu hizo zikiwa katika mawindo ya ubingwa, kuna vita mpya imeibuka kwa mastaa wa timu hizo na ile ya Singida Black Stars ikiongozwa na kinara, kiungo mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua.
Kiungo mshambuliaji huyo wa Simba ndiye kinara wa mabao katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu akiwa na mabao 16, matatu zaidi na waliyonayo nyota watatu wenye 13 kila moja akiwamo Clement Mzize na Prince Dube wa Yanga sambamba na Leonel Ateba wa Simba.
Ukiangalia orodha hiyo ya wafungaji, utabaini kuwa Ahoua ana nafasi kubwa ya kuibuka Mfungaji Bora kama atakomaa katika mechi mbili zilizosalia, ikizingatiwa anavaana na Kagera Sugar ambayo imeshashuka daraja mapema tofauti na wapinzani wake hasa wale wa Yanga, yaani Mzize na Dube.
Lakini ana vita ya chini chini dhidi ya Ateba ambaye anamiliki mabao matatu pungufu na aliyonayo Ahoua, kitu kinacholeta ushindani wa kushuhudia kile kilichotokea msimu wa 2020-21 wakati John Bocco alipompiku kiajabu, Chriss Mugalu dakika za jioni wakati akionekana kuibuka Mfungaji Bora.
Sio Ateba tu, lakini hata Steven Mukwala anayekipiga Msimbazi naye ana nafasi ya kufanya maajabu katika mbio hizo za ufungaji kwani ana mabao 12 na kama akitumia mechi mbili zijazo anaweza kumweka pabaya Ahoua na hata Ateba katika vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Vita kama hiyo ipo pia kwa Mzize nyota pekee mzawa anayechuana kibabe na mapro wa kigeni katika mbio za ufungaji bora kwa msimu huu, kwani naye ana vita ya wenyewe na Dube anayecheza naye katika kikosi cha Yanga, kila mmoja kwa sasa akimiliki mabao 13, lakini kuna Pacome Zouzoua anayemiliki 11 na anaonekana kuwa moto baada ya juzi kufunga mabao mawili walipoilaza Prisons 5-0.
Kule Singida Black Stars iliyojihakikishia nafasi ya nne na kukata tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao nako kuna vita ya wenyewe kwa mastaa wa timu hiyo, Jonathan Sowah anayemiliki mabao 12 na Elvis Rupia mwenye 11 ambapo yeyote atakayetumia dakika 90 zilizosalia kufungia msimu anaweza kuibuka mbabe.
Sowah aliyeanza kuitumikia Singida katika dirisha dogo akiitumikia katika mechi 13 amekuwa moto akitupia mabao hayo 12, wakati Rupia aliyekuwa ndiye kinara wa timu amepunguza kasi kwa kutoanza kikosi cha kwanza, lakini kasi ya ufungaji inambeba kwani mabao 11 aliyonayo sio haba.
Ramani nzima ya mbio za Mfungaji Bora kwa msimu huu itaonekana Jumapili baada ya kupigwa mechi nane za kukamilisha raundi ya 30, kisha kusubiriwa kiporo cha Dabi kuona ni nani atakayemrithi Stephane Aziz KI aliyenyakua kiatu cha dhahabu msimu uliopita kwa mabao 21 na asisti nane.
Aziz KI kwa sasa anakipiga Wydad Casablanca ya Morocco iliyomsajili hivi karibuni, huku akiwa ameifungia Yanga msimu huu mabao tisa na asisti saba.
WASIKIE WADAU
Mshambuliaji wa zamani wa Simba na Yanga, Hamis Kiiza ‘Diego’ akizungumzia mbio hizo za ufungaji alisema ushindani eneo la ushambuliaji linaendana na ubora wa ligi kwa sasa hivyo ni wazi kuwa Ligi ya Bara inakua na wachezaji wanaendana na ushindani uliopo.
“Eneo la ushambuliaji linatazamwa sana kwa sababu ndilo linaloamua matokeo hivyo ushindani uliopo ikiwa imesalia michezo michache na bingwa hajatangazwa ni wazi ushindani ni mkubwa na washambuliaji ndio wenye uamuzi wa taji hilo, hivyo naamini nafasi bado ipo wazi licha ya mmoja kutangulia kwa idadi ya mabao matatu,” alisema Diego na kuongeza;
“Mabao matatu kwenye mechi mbili kwa mshambuliaji mwenye jicho la kuona goli sio mengi sana. Siwezi kuzungumza nani atakuwa mfungaji bora kwa sasa yeyote kati ya hao anaweza kuwa mfungaji bora.”
Meneja wa Singida Black Stars, Amissi Tambwe aliyewahi kutwaa tuzo ya Mfungaji Bora kwa misimu miwili tofauti akiwa na Simba na Yanga, alisema safu za ushambuliaji zitaendelea kuonyesha makali hadi mchezo wa mwisho huku akimtaja Sowah kuwa kwake ndiye bora kutokana na kucheza mechi chache na kuingia kwenye ushindani.
“Sowah amecheza mechi 13 amefunga mabao 12 wastani ni kufunga kila mchezo. Kama angeanza mwanzo wa msimu angekuwa amefunga mabao mengi zaidi. Kwa kuzidiwa mabao manne tu na kinara, kwangu yenye ndiye bora.”