Matheo: Bwalya ni pengo Simba

Thursday June 23 2022
bwalya pic
By Olipa Assa
By Ramadhan Elias

STRAIKA wa KMC, Matheo Anthony amesema aina ya soka analocheza aliyekuwa kiungo wa Simba, Larry Bwalya ni mwiba kwa wapinzani, hivyo kuuzwa kwake anaona anastahili mbadala fundi zaidi yake.

Simba iliutumia mchezo dhidi ya KMC iliyopigwa mabao 3-1, kuagana na Bwalya aliyeuzwa Amazulu FC ya Afrika Kusini, baada ya kuwatumikia miaka miwili, ikimsajili kutoka Power Dynamos F.C 2020.

Matheo aliyasema hayo baada ya mechi yao na Simba, alimwelezea Bwalya jinsi akiwa na mpira inavyokuwa ngumu beki kumnyang’anya mguuni kwake na ufundi wa kupiga pasi.

“Bwalya anatumia akili kubwa kufanya kazi yake, kitu kikubwa hana papara ya kutoa pasi, faida nyingine akiwa anakabwa na wapinzani wengi anapunguza nafasi kwa wachezaji wenzake kuwa huru,” alisema Matheo na kuongeza;

“Simba itafute mbadala fundi kumzidi Bwalya atakayekuwa msaada kwenye michuano ya CAF ambayo inahitaji wachezaji wanaotumia akili zaidi kuzibeba timu zao.”

Mbali na kumzungumzia Bwalya, alisema msimu huu ni wa mafanikio kwake kufunga mabao nane na asisti tatu, hajawahi kufikisha idadi hiyo tangu aanze kucheza ligi.

Advertisement

“Yanga nilikuwa sipati nafasi ya kucheza hivyo sikuwa na mabao mengi, nikajiunga Polisi Tanzania 2019/20 ambako nilimaliza na mabao saba, 2020/21 dirisha dogo nilijiunga KMC nilimaliza na mabao matatu na sasa nina nane,” alisema.

Kaimu kocha mkuu wa Simba, Suleiman Matola alisema wanatafuta kwa haraka mbadala wa Bwalya, ili kuziba pengo lake, akikiri alikuwa muhimu kikosini.

“Vitu vya kujifunza kwa Bwalya ni nidhamu na bidii yake ya kazi, tunamshukuru kwa mchango wake na tunamuombea akafanye makubwa zaidi aendako,”alisema.

Kwa upande wa Bwalya alishukuru viongozi, makocha na mashabiki kwa ushirikiano waliompa tangu ajiunge nao, akisisitiza atawakumbuka daima.

“Haikuwa rahisi kuachana na Simba lakini imenibidi kwakuwa maisha ndivyo yalivyo. Simba imekuwa sehemu ya maisha yangu na imenipa vitu vingi ndani na nje ya uwanja vilivyonifanya kuwa boera kwa sasa,” alisema Bwalya.

Advertisement