Musonda Kutoka mikimbio hadi bao bora CAF

KATIKA dirisha dogo la usajili msimu huu, Yanga ilivuka boda hadi Zambia na kusajili mshambuliaji, Kennedy Musonda (29), kutokea Power Dynamos ya nchini humo.

Usajili wa nyota huyo ulionekana mkubwa kutokana na Musonda kuwa kinara wa upachikaji mabao katika ligi ya Zambia kwa wakati huo akiwa nayo 11, lakini jambo lingine lililofanya kuonekana usajili mkubwa ni mkwanja ambao alinunuliwa ambapo Power Dynamos ilivuna zaidi ya sh 150 milioni za kibongo.

Baada ya hapo alitua Bongo na kujiunga na Wananchi kisha kuanza kukichafua lakini punde si punde akajikuta akichambuliwa kama mchezaji mwenye 'Mikimbio mizuri', na sio hatari na baadhi ya Wadau wa soka.

Musonda ni kama aliwasikia lakini akakausha na kuamini katika miguu na akili yake na kuendelea kupiga matizi kwa juhudi ndani ya Yanga.

Muda ukasonga, akaanza kuaminiwa na kocha wa Yanga, Nassredine Nabi na kumpa nafasi kwenye baadhi ya mechi kisha kutengeneza pacha bora zaidi na straika Fiston Mayele.
Baada ya hapo akaanza kufunga, kwenye ligi ana mabao mawili lakini katika Kombe la Shirikisho afrika ambalo ndiko Yanga imeweka nguvu zaidi hivi sasa, amefunga mabao matatu na kutoa pasi za mwisho nne na kuwa miongoni mwa wachezaji waliohusika katika mabao mengi kwenye michuano hiyo.

Haikuishia hapo, bao alilofunga kwenye mchezo wa pili wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ugenini Afrika Kusini, dhidi ya Marumo Gallants likiwa la pili kwa Yanga ndilo likashinda tuzo ya bao bora la hatua hiyo.

Wakati bado watu wanamuweka kwenye muzani usiokuwa na usawa, Musonda huenda akaandika rekodi  mpya katika vitabu vyake vya Historia kwani ndani ya miezi sita aliyovaa jezi ya Yanga tayari amebeba Kombe la Ligi, na yuko fainali katika Kombe la Shirikisho Afrika, pia Kombe la TFF (ASFC).
Kama Yanga itaweza kutwaa mataji hayo mawili ambayo ipo fainali basi Musonda ataungana na wachezaji wenzake watatu, Metacha Mnata, Mudathir Yahya na Mamadou Doumbia kuwa mastaa waliobeba makombe matatu ndani ya miezi sita tu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Musonda alisema yupo Yanga kuhakikisha timu hiyo inatimiza malengo sambamba na ya kwake binafsi.

Pia Staa huyo alikiri kusikia maneno mengi mabaya  yanayozungumzwa kuhusu yeye lakini akasema hajali na anaamini ipo siku atawafunga midomo.

"Yanazungumzwa mengi kuhusu mimi ikiwemo kutopata muda mrefu wa kucheza.

Hayo hayaniwazishi kwani naamini mimi ni mchezaji wa Yanga na kocha ananiamini kwa asilimia kubwa hivyo kinachotokea ni mipango ya benchi la ufundi tu," alisema Musonda.
Kwa upande wa kocha Nabi alimzungumzia Musonda kama moja ya wachezaji bora katika kikosi chake huku akimtaja kama mpambanaji na mtu anayejituma zaidi.

"Musonda ni mchezaji mzuri, anapambana kuhakikisha timu inapata ushindi, ana matumizi mazuri ya nguvu, kasi pia ana uwezo wa kufunga pia anaweza kucheza eneo zaidi ya moja uwanjani. Nitaendelea kumtumia kwenye maeneo ambayo mpango wetu utamuhitaji kucheza," alisema Nabi.

Ikumbukwe Musonda asili yake ni mshambuliaji wa kati, namba tisa lakini kutokana na uwepo wa Mayele pale Yanga mara kwa mara amekuwa akitumika kama winga na wakati mwingine mshambuliaji wa pili na kufanya vizuri.