Nenda Jota nifikishie salamu kwa Maradona

Muktasari:
- Baba yako mzee Joaquim Silva mwenyewe amesimama kama mwanaume kumfariji mama yako Isabel Silva, lakini jambo baya ni kwamba wanaugulia mara mbili. Wanaugulia kwa kifo chako na wanaugulia kwa kifo cha mdogo wako uliyembeba, Andre.
WANASEMA mauti yamevikwa taji dhidi ya dua. Diogo Jota. Watu wamezungumza ya kuzungumza. Wamelia vya kutosha. Mkeo Rute Cardoso hajiwezi baada ya kusikia taarifa yako. Watoto wako hawajui chochote. Umezimika fundi.
Baba yako mzee Joaquim Silva mwenyewe amesimama kama mwanaume kumfariji mama yako Isabel Silva, lakini jambo baya ni kwamba wanaugulia mara mbili. Wanaugulia kwa kifo chako na wanaugulia kwa kifo cha mdogo wako uliyembeba, Andre.
Hakuna namna ya kukurudisha, sio kwa pesa wala uchawi. Ingewezakana hivyo Malkia Elizabeth wa Uingereza angekuwa hai. Nenda Jota ukimuona Diego Maradona mwambie Argentina imechukua tena Kombe la Dunia tangu ilipochukua mara ya mwisho mwaka 1986. Mwambie Cristiano Ronaldo na Lionel Messi kwa sasa hawachezi tena Ulaya.
Mwambie baada ya kufariki dunia, Napoli imebadilisha jina la uwanja na kuuita kwa jina lake - sasa unaitwa Stadio Diego Armando Maradona. Nenda Jota.

Mwambie Maradona familia yake bado inapambana mahakamani kuwashtaki manesi waliomhudumia kwamba, walifanya uzembe uliosababisha kifo chake. Mwambie kule Bunos Aires, Argentina na Naples, Italia katika kuta za mitaa mbalimbali kuna michoro ya sura yake. Najua unaweza kukutana na Edson Arantes do Nascimento ‘Pele’. Ukimuona mwambie Brazil yake sasa ni kama shamba la mahindi linalovunwa - watu wanajichukulia mabua wanavyotaka.

Ukimwona mwambie Neymar sasa amerudi Brazil bila ya Ballon D’or bali karudi na pesa na majeraha. Ukimwona Pele mwambie Brazil imebadilisha utararibu imeacha kiburi na imeanza kufundishwa na makocha kutoka nchi nyingine na sasa wana Carlo Ancelotti. Ukibahatika kumuona Mino Raiola mpe stori ya mtoto wake Paul Pogba. Mwambie sio Pogba yule tena.

Hakuna timu kubwa inayomtaka, majeraha ni sehemu ya maisha yake. Mwambie ni juzi juzi tu amessini mkataba na AS Monaco ambayo itamlipa Euro 350,000 kwa mwezi - pesa ambayo alikuwa akiipata kwa wiki.
Mwambie Raiola kwamba Erling Haaland anaendelea vizuri. Mwambie Rafael Pimenta aliyemwachia ofisi baada ya kifo chake anaendelea vizuri. Mwambie wachezaji aliowaacha wapo chini yake anawasimamia. Mpe pia habari za mchezaji wake Mario Balotelli. Mwambie kwa sasa naye anahangaika - amekuwa mchezaji wa bei rahisi sio yule aliyemwacha. Nenda Jota.

Mkumbushe tu, mpinzani wake Jorge Mendes kwa sasa sio tena wakala wa Cristiano Ronaldo. Mwambie kuna Messi mpya Barcelona anaitwa Lamine Yamal. Salamu ni nyingi pia ukimuona Marc-Vivien Foe mwambie rafiki yake Samuel Et’oo sasa ni rais wa Shirikisho la Soka Cameroon na anakabiliwa na tuhuma ya matumizi mabaya ya ofisi.
Ukikutana na Johan Cryf mjulishe kuwa ‘Total football’ yake inazidi kupamba moto, lakini Ajax yake inatia huruma.
Umemuachia huzuni nahodha wako wa timu ya taifa, Ronaldo kwa sasa machozi yake ya kukulilia yanamwagikia katika ardhi ya jangwa la Riyadh kule Saudi Arabia.

Umempa wakati mgumu Arne Slot nani atavaa viatu vyako? Kwa sasa mji wa Liverpool unazizima. Waingereza wameacha Uingereza wao wa kupenda vya nyumbani kwao - wote kwa sasa wanalitaja jina lako. Umempa kazi ngumu mtunza vifaa wa Liverpool, Lee Radcliffe. Ataanzaje kuondoa jina lako kwenye kabati la chumba cha kubadilishia nguo? Ni huzuni. Kwaheri Jota.
Kuondoka kwako kumewasahaulisha kidogo hata wachezaji wa Man United juu ya upinzani mkali uliopo baina ya timu zenu - wengi wameposti na kuonyeshwa kuumizwa juu ya kifo chako.
Umetuachia watoto watatu Denis, Dinis na Duarte. Hatujui kama watabarikiwa miguu ya ajabu kama yako, lakini tunaomba iwe hivyo. Hakuna aliyekuwepo wakati unavuta pumzi yako ya mwisho wakati moyo wako unadunda kwa mara ya mwisho, hivyo hatujui kauli ya mwisho ilikuwa ni ipi lakini sisi daima tutakukumbuka Diogo Jose Teixeira da Silva. Ukikutana nao wafikishie salamu zetu.