Azam Vs Simba utamu katikati ya ncha ya kisu

Monday May 13 2019

 

By THOMAS NG’ITU

MASHABIKI wa soka hasa wale ambao wapo kwenye mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, yaani kabla hata hawajafuturu watakuwa washajua nani mbabe baina ya Simba na Azam zinazovaana leo.

Wababe hao waliopishana kwa nafasi moja kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, watavaana kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam katika pambano la marudiano la Ligi Kuu Bara.

Hili ni pambano la 22 kwa timu hizo, kwani tangu Azam ilipopanda daraja msimu wa 2008-09, imeshakutana na Simba katika Ligi Kuu mara 21, huku Simba ikishinda mechi 10, Azam ikiibuka mbabe mara tano na mechi sita zilimalizika kwa sare.

Usichojua ni kwamba kwenye mashindano yote timu hizo zimeshakutana mara 34, huku Azam ikiburuzwa kwa kushinda 12 na kupoteza mechi 16 kwa Simba na mechi saba zikiisha kwa sare.

BOCCO NOMA

Katika mechi hizo zote, kinara wa mabao katika pambano la timu hizo ni John Bocco ambaye amefunga jumla ya mabao 20, akiyafunga akiwa Azam na kwa sasa akiwa na Wekundu wa Msimbazi.

Timu hizo zinakutana wakati Simba ikiwa kileleni mwa msimamo ikiwa na alama 81 baada ya kushuka uwanjani mara 32, huku Azam ikiwa nafasi ya tatu na pointi 68 kutokana na mechi 35.

Timu hizo zimetenganishwa na Yanga iliyopo nafasi ya pili ikiwa na alama 80 zilizotokana na michezo 35 iliyocheza mpaka sasa.

Katika mechi ya duru la kwanza iliyochezwa Feb 22, mwaka huu Azam ikiwa wenyeji wa pambano, matokeo yalikuwa 3-1, Simba ikitakata huku Bocco akitupia kambani lao lake la 20.

Kabla ya hapo Bocco alikuwa ametupia nyavuni mara 19 akifunga akiwa na uzi wa Azam akivalia jezi namba 19 ambapo Simba waliteseka juu yake kabla ya kumnyakua msimu uliopita.

MCHEZO MGUMU

Pambano la leo ni gumu, japo Azam hawana cha kupoteza katika Ligi Kuu kwani, hawana uhakika wa ubingwa kutokana na kutema alama nyingi wakati Ligi Kuu Bara ilipokuwa ikishika kasi.

Wanachofurahia ni kwamba wataicheza Fainali za Kombe la FA (ASFC) dhidi ya Lipuli Iringa na kama watashinda wana uhakika wa kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Mwanaspoti limeuangazia mchezo wa leo na kuona ugumu wake utakuwa katika bato ya wachezaji wa timu hizo na namna ambavyo kila mmoja anavyotaka kuweka heshima katika Ligi ya msimu huu.

Azam inataka kulipa kisasi cha kufungwa mechi mbili mfululizo kati ya tatu walizokutana katika Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili, tangu baadhi ya nyota wake akiwamo Bocco kuhamia Simba.

Nyota wengine ni Erasto Nyoni, Shomari Kapombe na kipa tegemeo Msimbazi, Aishi Manula na katika mechi za msimu uliopita timu hizo zilitoka suluhu mchezo wa kwanza na Simba kushinda 1-0 waliporudiana kabla ya msimu huu Azam kulala tena 3-1.

MANULA VS ABALORA

Hapa kila mmoja atataka kuonyesha umwamba kuwa, yeye ni bora kuliko mwenzake. Manula alisajiliwa na Simba akitokea Azam na ameonyesha uwezo mkubwa akiwa ndiye tegemeo.

Kwa upande wa Abalora, ambaye mabosi wake wameanza kumkatia tamaa naye ni mzuri, japo kwa siku za karibuni ameshuka na muda mwingine kufanya mambo mengi ya kitoto uwanjani.

Katika eneo hilo ni wazi kila mmoja kama watapangwa watataka kuonyeshana kazi na kuilinda timu yake isitoboke mbele ya mastraika wa timu hizo wenye uchu na lango.

AGGREY VS KAGERE

Hapa ni bampa tu bampa asikwambie mtu, Habari njema ni kwamba beki kisiki wa Azam Aggrey Moris amerejea kikosini baada ya adhabu yake ya kufungiwa mechi tatu na TFF kumalizika.

Kurejea kwake kutaongeza nguvu katika eneo la safu ya ulinzi la Azam lakini jambo jingine ni kwamba David Mwantika naye ameshaanza mazoezi takribani wiki na wenzake.

Beki huyu atakuwa na kazi ya kumzuia mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere aliye kwenye kiwango kizuri kwa akiongoza orodha ya wafungaji na mabao yake 20.

Morris atakuwa na kazi ya ziada kuonyesha umahiri wake katika kumzuia mshambuliaji huyo asiweze kuipenya ngome na kwenda kumtungua Abalora ama kipa yeyote atakayepangwa leo Uhuru.

UTAMU UPO HAPA

Asikwambie mtu babu, hii mechi itakuwa mechi ya kuchafuka katika eneo la kati kutokana na timu zote kuwa vizuri eneo hilo.

Simba ina James Kotei, Clatous Chama na Jonas Mkude viungo ambao wamekuwa katika kiwango kizuri katika msimu huu kwa kuweza kukaba wote na kupiga pasi kwa pamoja.

Lakini pia ina mafundi wengine kama Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin na Mohammed Ibrahim, bila kumsahau Haruna Niyonzima ambao yeyote atakayepangwa ni lazima waonyeshe shoo ya kibabe.

Upande wa Azam nako kumekucha kwani kuna Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya wakisaidiwa na Mcameroon Stephen Kingue ambaye ni mwanaume wa shoka katika kukaba.

CHIRWA VS MLIPILI

Katika safu ya ushambuliaji katika kikosi cha Azam huwezi kuliacha jina la Obrey Chirwa, ni mchezaji ambaye ameonyesha kiwango kikubwa tangu alivyojiunga nao katika dirisha dogo.

Chirwa akisaidiana na Donald Ngoma wamekuwa na ushirikiano mzuri katika eneo la ushambuliaji katika kuhakikisha kwamba wanapata magoli ya kuisaidia timu yao.

Mabeki wa Simba wakiongozwa na Yusuf Mlipili watakuwa na kazi ya ziada kuwazuia wachezaji hawa ni hatari akisaidiana na Nyoni, kwani Pascal Wawa na Paul Bukaba wote ni majeruhi.

Kwa hakika hili ni pambano usilotakiwa kulikosa.