Sababu tano zaipa Simba ubingwa TPL

Sunday April 21 2019

 

By CHARITY JAMES

SIMBA inaendelea kusafishiwa njia ya kutetea ubingwa msimu huu, hii ni baada ya wapinzani wao Yanga na Azam FC, kuzidi kuzidondosha pointi na wao kuzidisha kasi ya kutafuna viporo vya mechi zao. Yaani achana na matokeo ya mechi ya jana dhidi ya Kagera Sugar, Simba haijapoteza kiporo kabla ya jana.

Yanga ipo kileleni kwa pointi 74 katika mechi 32 walizocheza wameshinda 23, sare tano, wamepoteza nne ambapo sawa na kudondosha pointi 17, huku watani wao Simba wakiwa wamedondosha sita katika mechi 23.

Azam FC wao wamedondosha pointi 18 baada ya kucheza mechi 32, wameshinda 19 sare tisa wamefungwa mechi tatu, ambapo wamevuna pointi 66. Kwa mwenendo wa Simba kuonekana kufanya vyema kwenye viporo vyake kunawapa nafasi zaidi ya ubingwa kama watashinda mechi zote watakuwa na pointi 105 ambazo hazitaweza kufikiwa na wapinzani wao.

Mwanaspoti linakuletea mchanganua wa jinsi Simba ilivyo na nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu kutokana na namna inavyofanya vizuri.

VIPORO VINGI

Baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba wana ratiba ngumu inayowapa mapumziko ya siku mbili kila baada ya mechi na walianza dhidi ya Costal Union wakavuna pointi tatu wakishinda mabao 2-1 jana wameshuka dimbani kumenyana na Kagera yote michezo ya ugenini. michezo iliyobaki ni viporo dhidi ya Alliance Aprili 23, KMC hapo Aprili 26 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, Aprili 28 watakwenda Musoma kukipiga na Biashara na baadaye watakwenda Mbeya kukipiga na Tanzania Prisons na Mbeya City.

Advertisement

TIMU WANAZOKUTANA NAZO

Simba pamoja na kuwa kwenye ratiba ngumu, lengo la benchi la ufundi ni kupata matokeo ili kuhakikisha inatetea ubingwa wake. Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwa Kagera Sugar jana, Simba wanaonekana kuwa kwenye mtihani mkubwa watakapokuwa wakikutana na timu ambazo zipo katika hatari ya kushuka daraja.

Mchezo dhidi ya Biashara United, ambayo iko mkiani mwa msimamo, unatajwa kuwa mgumu kwa Simba huku ule dhidi ya Alliance FC nao ukiwapa presha kwani, hawako kwenye nafasi nzuri katika msimamo.

Biashara ina alama 34 baada ya michezo 31 huku Alliance ikiwa na alama 37 kwenye michezo 32 na iko nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi. Huku nyingine nyingi zikiwa katika nafasi ambazo hazina presha sana, lakini haziwezi kuwa mechi rahisi kwa Simba kwani kila mmoja anasaka ushindi ili kujihakikishia kubaki kwenye ligi.

KIKOSI WALICHONACHO

Msimu huu Simba ndio timu yenye kikosi bora na kinachosaka matokeo mazuri uwanjani. Achana na kasi yake ya kutafuna viporo, lakini Simba imedhihirisha hilo hata kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, wamekuwa na matokeo mazuri kwenye mechi zake zote za nyumbani na walitinga robo fainali kabla ya kukutana na kigingi cha TP Mazembe. Kwa sasa wamerudi Ligi Kuu wakiwa na maumivu ya kutolewa Ligi ya Mabigwa Afrika, na hasira ni kuzimaliza kwa kutoa vipigo kwa wapinzani wao kila wanapokutana.

Ikiwatumia wachezaji wake wenye viwango bora kwa sasa, Simba ina kikosi kipana na chenye kiu ya mafanikio kuanzia safu ya ulinzi hadi ushambuliaji hivyo, kinaweza kupindua meza muda wowote.

REKODI ZAO

Msimu uliopita Simba ilikuwa na rekodi nzuri katika Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, kwa kupata pointi zote sita kutoka kwa timu hizo mbili za jijini humo hivyo, kubebwa na rekodi katika michezo yake ijayo licha ya kwamba, lolote linaweza kutokea uwanjani.

YANGA, AZAM ZAIPA MWANYA

Yanga ilianza vizuri msimu huu kwa kutokuruhusu nyavu zao kutikiswa katika michezo yote ya mzunguko wa kwanza hadi walipovunjwa na Stand United kwa kuchapwa bao 1-0 kisha wakachapwa na Simba na baadaye Mtibwa Sugar na Lipuli FC.

Kasi ya Yanga ilikuwa tishio kwa Simba ambao, walikuwa wanaomba kila siku kupoteza mechi zao ili kuwapa nafasi ya kutetea taji lao.

Hata hivyo, Simba watakuwa kwenye wakati mgumu kuhakikisha inashinda mechi zake za viporo ili kufikia malengo yake kwa msimu huu.

Achana na Yanga sasa kuna ishu ya Azam FC ambayo pia ilikuwa na rekodi nzuri katika michezo ya mwanzo, lakini wanaonekana kukata pumzi na kushindwa kufikia malengo na sasa wameanza kujiengua kwenye ramani ya ubingwa, baada ya kushindwa kutumia vizuri michezo ya ugenini.

MAKOCHA WAMEFUNGUKA

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema mpira sio mchezo wa hesabu ni pointi ambazo zinapatikana ndani ya dakika 90 na kama wamepoteza hata hao wapinzani wao wanaweza kupoteza vivyo hivyo.

Hata hivyo, alisema kuwa suala la kusaka ubingwa bado lipo pale pale na hawajakata tamaa hadi mwisho. Zahera, ambaye alianza msimu mpya kwa rekodi ya kutofungwa, alisema atapambana hadi mwisho mwa msimu kuona bingwa anaamuliwa kwa pointi.

“Unajua soka linachezwa uwanjani nani alitegemea kama tutafungwa namna ambavyo tulianza kwa kushinda kila mchezo, hivyo msiniambie mpira wenu wa midomoni nasubili ligi ikiisha ndio majibu yatapatikana nani anafaa kutwaa ubingwa na nani hafai.

“Nina mchezo mgumu mbele na jana tumeanza mazoezi baada ya kupumzika kwa muda tukitoka kupoteza dhidi ya Mtibwa na kuna makosa walifanya wachezaji wangu, ninayafanyia kazi kabla ya mchezo na Azam FC lengo ni kupata matokeo mazuri,” alisema.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila amesema soka ni mchezo wa makosa na wao wamekosea na wamejitoa katika mbio za ubingwa na wanaipa nafasi kubwa Simba kutetea ubingwa wake msimu huu.

Alisema ni ngumu kumtaja bingwa kwa sasa kutokana na Simba kuwa na viporo vingi na Yanga kucheza michezo mingi iliyompa pointi, kwa sasa anasubiriwa mpinzani wake aweze kumaliza viporo ndipo bingwa atajulikana.

“Huwezi ukasema Simba bingwa kwa sababu ana viporo vingi, sio kweli mtu akiwa na pointi tayari ndio mshindi na anayetegemea kucheza kwanza anaweza akapoteza na akaachwa, lakini nafasi nazipa timu hizo mbili,” alisema.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Meja Mstaafu, Abdul Mingange amesema anawapa nafasi kubwa Yanga kwa sababu wana pointi nyingi mkononi na mchezo wao wa Aprili 29, unaweza kuwamua ubingwa msimu huu.

“Yanga wana pointi, Simba wanasubiri kuzipata baada ya kucheza lakini kwa uhalisi aliye na pointi ndio bingwa. Kwa upande wetu tunagombania nafasi ya pili ambayo maamuzi ya kufikia lengo ni kushinda michezo yetu yote ukiwemo wa Yanga ambao, na wanasaka alama tatu muhimu,” alisema.