NYUMA YA PAZIA : Zlatan angerudisha nyuma nyakati akutane na wenzake

Muktasari:

Nakukumbusha nyakati ambazo mpira ulikuwa unatawaliwa na wababe. Sio tu England lakini mpira ulitawaliwa na wanaume. Soka haukuwa mchezo wa watu laini. Ulikuwa mchezo wa wanaume haswa. Nyakati zimeondoka.

WABABE? Waliisha zamani. Nakumbuka jinsi Steven Gerrard akiwa kinda alivyoachiwa funguo za gari na Paul Ince. Gari la kifahari. Paul Ince alikuwa amesahau kitu akamtuma Gerrard aliyekuwa mtoto akifuate. Gerrard alikuwa hawezi kuendesha gari.

Pamoja na kutoweza kuendesha gari lakini hakuwa na uwezo wa kurudi kwa Ince kumwambia alikuwa hajui kuendesha gari. Angemkabili vipi Ince? Hakujua. Alichofahamu ni asingejua Ince angemjibu nini au angemfanya nini kwa kurudi na kumwambia hawezi kuendesha gari.

Nyakati hizo wachezaji walikuwa wababe. Hapa nakusimulia Ince ambaye alikuwa amerudi England kucheza Liverpool akitokea Inter Milan ya Italia. Kabla ya hapo kumbuka Ince alikuwa Manchester United. Sir Alex Ferguson alilazimika kumuuza Ince kwa sababu asingeweza kuwa na wababe wawili katika chumba kimoja cha kubadilishia nguo. Kando ya Ince kulikuwa na Roy Keane.

Nakukumbusha nyakati ambazo mpira ulikuwa unatawaliwa na wababe. Sio tu England lakini mpira ulitawaliwa na wanaume. Soka haukuwa mchezo wa watu laini. Ulikuwa mchezo wa wanaume haswa. Nyakati zimeondoka.

Wachezaji walikuwa wababe. Makocha wababe. Mashabiki wababe. Waamuzi kina Perluigi Collina walikuwa wababe. Kila mtu alikuwa mbabe. Bahati mbaya mchezo umekuwa laini na unashangaa wanapojitokeza watu wagumu katika mchezo laini. Unatamani urudishe nyuma nyakati na kuwaingiza wagumu wa sasa katika nyakati ngumu za sasa.

Nilikuwa namtazama Zlatan Ibrahimovic wiki tatu zilizopita nikakumbuka kitu. Zlatan anapenda ubabe kweli kweli lakini kwa nini haishi katika zama zake? Wiki hii ameaga kibabe pale LA Galaxy. Ubabe mwingi kweli kweli.

Kaweka picha yake kubwa katika ukurasa wake wa Instagram kisha akaandika. “Nilikuja, niliona, nikatawala. Kwa mashabiki wa Galaxy, mlimtaka Zlatan, mkapewa Zlatan. Mnakaribishwa sana. Stori inaendelea. Haya sasa nendeni mkatazame Baseball.”

Ahh Zlatan bwana. Hapa alikuwa anamaanisha baada ya yeye kuondoka hakuna soka tena Galaxy. Dharau kwa wenzake. Bingwa wa majigambo. Mbabe. Lakini hapa katika ubabe Zlatan ana historia ya ubabe haswa.

Ana mkanda mweusi wa karate. Aliupata kwao Sweden. Haishangazi kuona anapiga mabao maridadi ya kujipindua hewani. Lakini haishangazi kuona jinsi anavyotembeza ubabe katika vyumba vya kubadilishia nguo katika klabu alizopita.

Ndani na nje ya uwanja Zlatan ni mbabe kwa wenzake. Akiwa na PSG, aliwahi kumwambia staa mwenzake, Gregory van der Wiel ‘Sikiliza cheza vizuri sitakupiga, sawa?’ Hii ndio mikwara ambayo Zlatan huwa anatembeza uwanjani.

Hapo hapo PSG aliwahi kumsimamia Lucas Moura na fimbo wakati wakiwa Gym. Akamchapa fimbo za tumboni kwa ajili ya kumrekebisha. Huyu ndiye Zlatan mbabe wao. Hawawezi kumrudishia kitu. Mtu pekee wa zama hizi aliyejaribu kusimama naye alikuwa staa mwenzake wa AC Milan, Oguchi Onyewu.

Huyu jamaa wazazi wake ni Wanigeria lakini amezaliwa Washington Marekani. Ana urefu wa futi 6.5 kama ilivyo kwa Zlatan. Katika ugomvi wao wa mazoezini Zlatan anakiri alivunjwa mbavu na Onyewu. Pengine ndio pambano alilopoteza mpaka sasa.

Vinginevyo natamani kumwona Zlatan katika kizazi cha wagumu wa zamani. Kwa sasa ni kama anaonea. Wakati akiwa na Manchester United alikuwa anawapiga kabali kina Jesse Lingard. Hawafikii walau mabega ya Zlatan.

Sio kina Lingard tu, kokote ambako Zlatan alipita makinda walijikuta katika wakati mgumu kumtazama usoni na kumvimbia Zlatan. Kisa? Ubabe wake. Majivuno yake. Wajihi wake. Nadhani Zlatan alipishana na zama fulani hivi.

Ingekuwa raha kama Zlatan angechangia chumba cha kubadilishia nguo na kina Keane, Ince, Patrick Vieira, lakini zaidi na mtu kama Duncan Ferguson. Unamkumbuka Big Dan? Alikuwa pale Everton. Siku moja nyumbani kwake alivamiwa na wezi wawili. Mwizi mmoja alifanikiwa kutoroka, mwingine akaishia katika kitanda cha hospitali.

Kulikuwa na kina Thomas Repka. Pale Wimbledon kulikuwa na mtu kama Vivie Jones. Ukubwa wake wa mwili na ubabe wake ukasababisha watu wa Hollywood wamchukue. Unapomfikiria mtu kama Zlatan na ubabe wake wa kileo, unatamani angecheza katika zama zile. Nadhani kuna kiburi angepunguza.

Pale Denmark walikuwa na mtu aliyeitwa Stig Tofting. Alikuwa zaidi ya wacheza mieleka unaowaona kwa sasa kina John Cena. Ugomvi aliununua kwa bei nafuu. Aliwahi kwenda jela kwa siku 20 kwa kuchakaza watu katika ugomvi wa barabarani. Natamani Zlatan angekutana na watu hawa kujipima ubavu wake.

Tatizo mchezo wenyewe umekuwa laini. Sio mgumu tena. Zlatan anajaribu kutulazimisha kweli kweli turudi katika zama za ubabe na majigambo lakini nadhani hatuwezi kurudi huko. Tunachotamani ni kama mwenyezi Mungu angeweza kurudisha nyuma nyakati na kumtia katika zama kama zile za wale Wajerumani wa wakati ule.

Unawakumbuka? Stefan Effenberg. Jens Jeremies. Mario Basler. Kapteni Lothar Mattheuas na wengineo. Angejipima ubavu na wenzake sio hawa wa leo.