Zidane analo kwa Messi

BARCELONA ,HISPANIA. MAMBO iko Nou Camp leo Jumamosi. Zinedine Zidane na chama lake la Real Madrid watakwenda kukabiliana na Lionel Messi na jeshi lake katika mchezo wa kwanza wa El Clasico kwenye La Liga msimu huu utakaopigwa Nou Camp.

Madrid inakwenda kwenye mchezo huo ikiwa kwenye kiwango duni cha soka lake, ikitokea kupoteza mechi mbili mfululizo, dhidi ya Cadiz kwenye La Liga na Shakhtar Donetsk kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mechi hizo zote mbili, Los Blancos ilichapwa kwenye uwanja wake wa nyumbani. Hivyo, kipigo cha tatu mfululizo, tena kutoka kwa mahasimu wao Barcelona, kinaweza kuwa habari mbaya kwa kocha huyo Mfaransa.

Hata hivyo, El Clasico ya msimu huu itakosa huduma za mastaa wa maana, Gareth Bale kwa upande wa Real Madrid na Luis Suarez kwa upande wa Barcelona. Wakali hao wote wamebadili timu kwenye dirisha lililopita, Bale akirudi zake Tottenham kwa mkopo na Suarez ameuzwa Atletico Madrid.

Zidane hajafungwa Nou Camp

Wakati Zidane akisaka matokeo ya lazima huko Barcelona, rekodi za Zidane zinaonyesha dhahiri kwamba hajawahi kupoteza mechi Camp Nou, mara zake tano alizokwenda uwanjani hapo. Kwenye karatasi, Real Madrid wanaonekana hawapo vizuri, lakini Madrid ya Zidane imekuwa na kumbukumbu tamu Nou Camp. Zidane amekabiliana na Barcelona mara tisa, amepoteza mara mbili akiwa kocha na zote uwanjani Santiago Bernabeu. Rekodi ya kushinda mechi nne na sare tatu inawatisha Barcelona linapokuja suala la kukabiliana na Zidane. Mechi yake ya kwanza ya El Clasico uwanjani Camp Nou ilikuwa Aprili 2, 2016 ambapo ilitibua kasi ya Barcelona kushinda mechi 39 na kulipa kisasi cha kipigo cha 4-0 wakati Madrid ilipokuwa chini ya Rafael Benitez. Los Blancos ilikuwa pungufu baada ya Sergio Ramos kutolewa kwa kadi nyekundu, lakini Cristiano Ronaldo alimaliza mechi. Zidane hajapoteza mechi Camp Nou.