Zahera kuishuhudia Yanga, Polisi Tanzania jukwaani

Muktasari:

Benchi la ufundi la Yanga kesho litakuwa  chini ya kocha msaidizi Noel Mwandila akisaidiana na kocha wa makipa Peter Manyika

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera kesho Alhamis ataanza kutumikia adhabu yake ya kutokukaa benchi akitumikia adhabu yake na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kushindwa kufuata sheria za mavazi kwa benchi la ufundi.

Yanga inashuka uwanjani kesho kumenyana na Polisi Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania bara ukiwa ni mchezo wake wa pili baada ya kuanza na Ruvu Shooting na kupoteza kwa kufungwa bao 1-0.

Akizungumza Dar es Salaam leo, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli alisema kocha atashuhudia mchezo huo akiwa jukwaani.

"Adhabu ya kufungiwa mechi tatu anatarajia kuianza kesho na dhidi ya Polisi pamoja na ule wa Coastal Union Jumapili kabla atujaanza safari ya Kanda ya Ziwa ambapo pia atakosa mchezo mmoja," alisema Bumbuli.

Bumbuli alisema kikosi kesho kitakuwa chini ya kocha msaidizi Noel Mwandila akisaidiana na kocha wa makipa Peter Manyika.