Zahera aukubali mziki wa Simba

Thursday October 01 2020
zaheraa pic

MKURUGENZI wa ufundi wa timu ya Gwambina FC, Mwinyi Zahera amesema Simba ilistahili ushindi kwenye mechi waliyokutana kwasababu waliwazidi kimchezo.

Katika mechi hiyo Simba ilishinda mabao 3-0, Zahera amedai safu yao ya ushambuliaji bado haijakaa sawa na kusababisha kutopata matokeo mazuri.

"Katika mechi tulizocheza, Simba tu ndio walipata ushindi halali kwa sababu walituzidi kila idara, lakini wengine walibebwa na bahati hivyo naamini kadri tunavyokwenda timu itabadilika," amesema Zahera.

Gwambina ndio timu pekee ambayo haijafunga bao hadi sasa kama ilivyo kwa Mbeya City, imeshacheza mechi nne ambapo imepoteza mitatu na sare moja na Jumamosi Oktoba 3 itakuwa nyumbani kuwakaribisha Ihefu, mchezo utakaopigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.

Zahera amesema pamoja na kutopata matokeo mazuri, lakini timu imekuwa ikicheza vizuri isipokuwa tatizo lipo katika sehemu ya ushambuliaji kwa kushindwa kutumia vyema nafasi wanazopata.

Amesema tatizo lingine ni kutokana na kukosa uzoefu kwa baadhi ya nyota wao, huku akibainisha kuwa katika mwendelezo wa Ligi, Gwambina itabadilika na kufanya vizuri.

Advertisement

Zahera pia ameeleza kutohusika katika upangaji kikosi, huku akieleza anawaachia Kocha Mkuu na Msaidizi wake licha ya kwamba anafuatilia kwa ukaribu mazoezi ya kila siku na kwamba kazi yake kubwa ni kuhakikisha anasimamia programu.

Advertisement