Zahera: Asiyekuja mazoezini kesho hachezi tena Yanga

Thursday April 25 2019

 

By Charity James

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amewapiga mkwara wachezaji wote waliogoma kufanya mazoezi endapo watashindwa kufika mazoezini kesho hawataichezea tena timu hiyo hadi mwisho wa msimu.

Katika onyo hilo la Zahera halitawagusa wachezaji wawili  pekee Kelvin Yondani, Papy Tshishimbi.

Katika ujumbe wake aliotuma katika mitando ya kijamii leo Zahera alisema katika maisha yake yote ya ufundishaji hajawahi kuwasimamia wachezaji kama anavyofanya Yanga, lakini anashangazwa na uamuzi waliochukua bila ya kumpa taarifa.

"Wachezaji wa Yanga nadhani maisha yao yote awata pata mtu kama mimi nimekuwa nikiwasaidia mambo mengi ndani na nje ya uwanja pamoja na maisha yao tangu nimefika ndani ya hii timu nimesikitishwa na hiki walichokifanya bila ya mimi kushirikishwa."

"Baada ya kukosa mazoezi leo nimeongea na Hafidh Saleh kuwaambia kuwa kwa yeyote atakayekosa mazoezi ya kesho asirudi tena kwenye kikosi changu kwani haiwezekani wachezaji wakaanza kugomea mazoezi mwezi mmoja kabla ya ligi kumalizika," alisema Zahera.

Zahera alisema ameshangazwa na wachezaji hao kugomea mshahara huku Ligi ikiwa imebakiza mwezi mmoja kuisha, wakati walikuwa wakipata kama kawaida.

Advertisement

"Sio leo kwamba ndio wanakosa mshahara, walikuwa wanapata mshahahara ebu waulizeni mara ya mwisho lini walipata mshahara iweje wagome sasa?," alihoji kocha huyo.

Advertisement