Yondani atua Namungo

Muktasari:

Kelvin Yondani kabla ya kuitumikia Yanga, alikuwa akiichezea Simba tangu mwaka 2006 mpaka alipokwenda Yanga aliyoitumikia kwa miaka nane na kutua Namungo.

Beki mkongwe nchini, Kelvin Yondan amesajiliwa kwa mkataba wa mwaka mmoja na Namungo ya Ruangwa mkoani Lindi.

Yondani aliachwa na Yanga mara baada ya msimu uliopita kumalizika kwa maana hiyo Namungo wamemsajili kama mchezaji huru.

Yondani aliyeitumikia Yanga kwa miaka nane tangu mwaka 2012, alishindwa kuongeza mkataba na timu hiyo kutokana na kushindwa kuelewana katika masuala ya kimaslahi.

Namungo wataanza kumtumia Yondani ambaye ni mchezaji huru mwezi Novemba.

Katibu Mkuu wa Namungo, Ally Selemani amesema wamemsajili beki huyo mzoefu ili kuboresha eneo lao la ulinzi.

Selemani anasema wanachosubiri ni kuangalia utaratibu wa kumtumia Yondani kama sheria za Ligi Kuu Bara zinavyotaka.

"Muda wa mkataba ambao tumemsajili Yondani ni mwaka mmoja kama mambo yatakuwa vizuri tunanafasi ya kumuongeza mwingine ndani yake au utakapo malizika," anasema.

"Bado tupo tunaijenga timu yetu kama ambavyo benchi la ufundi litakuwa linahitaji na katika kuhakikisha hilo tumemchukua Yondani kama mchezaji mwenye uwezo na uzoefu," anasema.

"Tunaweza kushtua tena kwa kunasa kufaa kingine kama mambo yatakuwa mazuri dhidi yetu na mchezaji huyo mwenye uwezo na uzoefu kama Yondani.

"Ukiangalia bado ligi msimu huu hatujaanza vizuri pengine kutokana na kikosi chetu kuwa kipya lakini baada ya muda mambo yatakuwa mazuri wala hatuna wasiwasi na hilo," anasema Selemani.

Katika kuendelea kusuka kikosi cha Namungo, jana wachezaji waliocheza dhidi ya Tanzania Prisons nyota Adam Salamba aliingia akitokea benchi.