Yanga yaweka Mil 900 mezani

Muktasari:

YANGA imetumia dola 400,000 sawa na Sh924 milioni kusuka kikosi chake kipya kilichopo kambini Kigamboni, Jijini Dar es Salaam.

YANGA imetumia dola 400,000 sawa na Sh924 milioni kusuka kikosi chake kipya kilichopo kambini Kigamboni, Jijini Dar es Salaam.

Klabu hiyo ambayo inaanza msimu kwa kucheza ya Prisons ya Mbeya keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa, imesajili mastaa wapya 12 ambao wameungana wa zamani kuunda kikosi cha wachezaji 27.

Mastaa ghali wa nje ambao Yanga imetumia nguvu kubwa na jeuri ya fedha kuwasajili ni winga Tuisila Kisinda akifuatiwa na kiungo Mukoko Tonombe wote wakivunjiwa mikataba kwa GSM katika klabu yao ya zamani ya AS Vita.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga ni kwamba wachezaji hao wawili wa DR Congo wameigharimu klabu zaidi ya Sh 250Milioni kunasa saini zao kibabe na tayari usajili huo tu umeshazalisha bao moja la winga Kisinda alilofunga siku ya Mwananchi na kubaki midomoni mwa mashabiki.

Mbali na gharama hizo pia wachezaji hao pamoja na wengine wapya waliosajiliwa msimu huu viwango vyao vya mishahara ni vikubwa tofauti na waliokuwapo msimu uliopita ingawa Yanga wanafanya siri kubwa.

Nyuma ya Wakongomani hao wapo kiungo Carlos Fernandes ‘Carlinhos’ ambaye ametua Yanga akiwa mchezaji huru akitokea Angola sambamba na mshambuliaji Mghana Michael Sarpong na Yacouba Sogne wa Burkina Faso.

Yanga imebakiza nafasi mbili za wachezaji wa kigeni ambazo inaelezwa moja itatumika baadaye kwa staa mmoja mkubwa atakayeshtua soka la Tanzania huku nyingine akiachiwa Kocha Zlatko Krmpotic kuchagua mtu anayetaka kumuongeza.

Mastaa wazawa mchezaji ghali ni beki Bakari Nondo Mwamnyeto ambaye Yanga ilishinda vita ya kumsajili kutoka katika mikono ya Simba waliopambana kumsajili lakini wakapigwa bao jioni.