Yanga yamrudisha Ninja rasmi

Muktasari:

Beki Abdallah Shaibu 'Ninja' amerejea Yanga baada ya kuachana nayo kwa miaka miwili alipotimkia Canada kisha kurejea nchini.

Yanga imemrejesha rasmi beki wao wa zamani Abdallah Shaibu 'Ninja' akitokea MFK Vyskv ya Czech.

Ninja amesaini mkataba wa miaka miwili leo ukiwa ni usajili wa tatu wa Yanga kwa upande wa mabeki akitanguliwa na Bakari Mwamnyeto (kutoka Coastal Union) na Yassin Mustapha (kutoka Polisi Tanzania) na wanne kwa wachezaji wote waliosajiliwa.

Amesaini mkataba huo mbele ya Makamu Mwenyekiti Frederick Mwakalebela aliyeambatana na kaimu katibu mkuu wa klabu hiyo Simon Patrick.

Awali Ninja alionekana akijifua na kikosi cha timu hiyo mara baada ya kurejea kutoka Czech na kuonekana ni wazi alikuwa akiangaliwa kwa lengo la kusajiliwa.

Beki huyo ambaye amewahi kuitumikia kwa mkopo LA Galaxy anarejea Yanga baada ya kuachana nayo kwa miaka miwili kufuatia mkataba wake kumalizika.

Yanga imelazimika kumsajili Ninja baada ya kukosa saini ya beki mwingine wa Coastal Union Ibrahim Ame ambaye juzi alisainishwa kimafia na Simba ikimchukua juu kwa juu wakati akiwasili bandarini akitokea Zanzibar.