Yanga walivyotegua mtego

Wednesday October 28 2020
yanga2 pic

YANGA imeshacheza mechi sita mpaka sasa ikipoteza pointi mbili pekee katika idadi hiyo ya dakika 540 uwanjani.

Lakini, dakika hizo wamezicheza kimkakati kufuta matokeo yaliyowanyima ubingwa msimu uliopita, huku macho yote sasa yakiwa kwa Biashara United ya Musoma.

Iko hivi. Katika mechi saba ambazo imecheza mpaka sasa hakuna timu ambayo iliifunga mara mbili ambapo zote ziliitibulia kama sio mchezo mmoja ni yote miwili. Sasa wameanza nazo kwa kuzichapa na kutegua mitego hiyo inayoweza kuwanyima ubingwa mapema.

Yanga ilifungua ligi kwa sare ya bao 1-1 ikiwa nyumbani dhidi ya Prisons, ukiwa ndio mchezo pekee waliangusha pointi mpaka sasa, lakini askari hao waliwatibulia hata msimu uliopita. Msimu uliopita Prisons na Yanga walianzia ugenini ambapo vijana hao wa Magereza walikubali kipigo cha bao 1-0, lakini baadaye waligoma kufungwa na kutoa suluhu nyumbani.

Yanga ikapindua meza msimu huu kwa kuanza na ushindi nyumbani dhidi ya Mbeya City ambao msimu uliopita waligawana pointi katika mechi zote mbili wakitoa sare. Mtibwa Sugar ambao walivuna pointi moja kwa Yanga msimu uliopita, msimu huu tayari wameshapasuka nyumbani kwa bao 1-0 wakisubiri mchezo wa pili, huku msimu uliopita wakipoteza ugenini kisha kuwalazimisha sare kwao.

Upande wa Coastal Union ambao nao waliambulia pointi moja msimu uliopita, ni kama Mtibwa Sugar ambapo wamepoteza mechi ya kwanza ugenini kwa mabao 3-0 ikiwa ni mechi ambayo Yanga imevuna mabao mengi mpaka sasa na wanasubiri kurudiana.

Advertisement

Yanga pia imepindua meza kwa kushinda nyumbani dhidi ya Polisi Tanzania ambayo katika uwanja huo msimu uliopita ililazimishwa sare ya mabao 3-3, lakini pia mchezo wa marudiano walilazimishwa sare ya bao 1-1 ugenini.

KMC ambayo msimu uliopita ilivuna pointi nne kwa Yanga, msimu huu imeshatibua rekodi yake ambapo Yanga imewafunga juzi kwa mabao 2-1.

Hata hivyo, Biashara United ndio timu pekee iliyoshikilia hatima ya Yanga inayofundishwa na Cedric Kaze kupanda kileleni katika msimamo wa ligi endapo itashinda ugenini Oktoba 31.

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba ‘Tekelo’ amedai kwamba kwa kasi ya Yanga inaonyesha benchi la ufundi limejifunza kitu katika kuangalia ubora wa wapinzani msimu huu, lakini pia wakiyahusisha na ya nyuma. “Ukiangalia Yanga wanaonekana kujifunza kitu katika kufuatilia ubora wa wapinzani wao msimu huu, lakini kikubwa pia wamekuwa wakiangalia jinsi walivyowasumbua na kujipanga kupata ushindi.

“Hatua nyingine hapa tunapata picha kwamba msimu huu Yanga kuna kitu wamebadilisha katika kikosi chao ambacho kinawapa ubora wa kupata matokeo, lakini pia naona timu pinzani wanazokutana nazo hazijabadilika sana. Hii inaweza kuwa faida kubwa kwa Yanga,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars.

Alisema kimkakati wanachokifanya Yanga ni muhimu zaidi kuelekea kwenye mbio za ubingwa kwani kwa hali ilivyo msimu huu, ukipoteza pointi moja kuirudisha ni shughuli na anaamini kwamba Yanga iko kwenye wakati mzuri.

AZAM WAMETELEZA

Wakati Yanga wakiendelea na karata zao, kizuizi kikubwa kwa timu hiyo kinaweza kuwa vinara wa Ligi Kuu, Azam, ambao wamekuwa na ubora wakizifunga timu ambazo ziliwasumbua msimu uliopita ingawa juzi walipoteza mchezo wa kwanza.

Azam ilipoteza katika ligi wakiwa ugenini wakikubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar matokeo ambayo ni wazi yamewashtua wakiwa na mwanzo mzuri wa ligi.

Kabla ya matokeo hayo, Azam ndio waliokuwa wanaonekana timu tishio msimu huu wakiwa na kasi ya kushinda mechi zote za nyumbani na ugenini - matokeo yaliyowaweka kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Uongozi huo wa ligi unaweza kufikia kikomo kwa matajiri hao endapo Yanga itashinda dhidi ya Biashara United ambayo Yanga hawakuwahi kuifunga tangu wapande Ligi Kuu ambapo matokeo mazuri kwao wakia ugenini dhidi ya Biashara wakiwa ugenini yamekuwa ni kupata sare.

Pia Azam imeshinda zote za nyumbani, lakini hatua kubwa ni kuifunga Kagera Sugar ambayo msimu uliopita iliambulia pointi moja katika Uwanja wa nyumbani wa vinara hao wa ligi.

SIMBA IMEYUMBA

Simba ambao ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, msimu huu wameshapoteza mechi mbili na sare moja katika mechi zao nane za kwanza jambo ambalo sio la kawaida kwao, huku nahodha John Bocco akiomba radhi kwa mashabiki.

Simba imepoteza dhidi ya Prisons kwa bao 1-0 katika mchezo wa ugenini ambapo timu hizo mbili katika msimu uliopita ziligawana pointi kwenye mechi zote mbili za nyumbani na ugenini.

Wekundu hao pia walijikuta wanapoteza mechi ya pili mfululizo baada ya juzi kufungwa nyumbani dhidi ya Ruvu Shooting ambao hawakuwahi kuifunga Simba katika misimu ya hivikaribuni.

Hali mbaya ya Simba ikajidhihirisha pia walipotoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar ambayo msimu uliopita wekundu hao walishinda mechi zote mbili. Wekundu hao mpaka sasa wameshapoteza pointi tatu dhidi ya Prisons ya jijini Mbeya ambayo msimu uliopita waligawana nayo pointi katika mechi zote mbili.

 

Advertisement