Yanga, Polisi Tanzania ni mshikemshike leo Uwanja wa Uhuru

Muktasari:

Kocha huyo amekuwa na rekodi nzuri ya kushinda dhidi ya Yanga tangu akiwa Lipuli ya Iringa. Katika mechi tatu ambazo amekutana na Yanga mwaka huu ameshinda zote. Machi 16 akiwa Lipuli alishinda bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu

Dar es Salaam. Yanga inaikabili Polisi Tanzania ikiwa na mambo matatu ambayo inatakiwa kuyafanyia kazi ili kupata ushindi katika mchezo wa leo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Yanga inacheza mchezo wa pili katika mashindano hayo baada ya ule wa ufunguzi kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting.

Mchezo wa leo utakuwa wa kwanza kwa Yanga tangu iliporejea ikitokea katika Ligi ya Mabingwa Afrika ilipotolewa na Zesco ya Zambia kwa kufungwa mabao 2-1.

Mambo matatu yanayoikabili Yanga leo ni rekodi nzuri ya Kocha wa Polisi Tanzania Selemani Matola, safu isiyokuwa imara ya ushambuliaji na kushika mkia katika Ligi Kuu ikiwa haina pointi.

Matola

Kocha huyo amekuwa na rekodi nzuri ya kushinda dhidi ya Yanga tangu akiwa Lipuli ya Iringa. Katika mechi tatu ambazo amekutana na Yanga mwaka huu ameshinda zote. Machi 16 akiwa Lipuli alishinda bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu. Mei 6 Lipuli ilishinda mabao 2-0 katika mchezo wa Kombe la Shirikisho (FA) kabla ya Agosti 16 kuilaza 2-0 akiwa Polisi Tanzania katika mchezo wa kirafiki.

Mbali na rekodi ya Matola, Polisi Tanzania ina washambuliaji wazoefu  Marcel Kaheza na Ditram Nchimbi.

Kaheza amewahi kucheza Majimaji na Simba wakati Nchimbi aliwahi kutamba Mbeya City, Njombe Mji, Azam na Mwadui kabla ya kutua Polisi Tanzania.

Uwezo wa Kaheza na Nchimbi unaweza kuipa wakati mgumu ngome ya  Yanga ambayo itakuwa chini ya Kelvin Yondani na Lamime Moro.

Kocha Mwinyi Zahera anaweza kuendelea kuwaamini mabeki Ally Ally na Ally Sonso kucheza pembeni.

Zahera atakuwa jukwaani akitumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu na Kamati ya Bodi ya Ligi Kuu ya Uendeshaji na Usimamizi kwa madai ya kutoa matamshi yasiyofaa kwa taasisi hiyo. Noel Mwandila ataongoza kikosi.

Washambuliaji

Yanga inacheza na Polisi Tanzania ikiwa haina rekodi ya kuvutia katika kufunga mabao msimu huu. Katika mechi nne za kimataifa na Ligi Kuu, Yanga imefunga mabao manne.

Licha ya safu hiyo kuundwa na asilimia kubwa ya wachezaji wa kigeni, Juma Balinya, Patrick Sibomana, Sadney Urikhob na David Molinga, Yanga haina muunganiko mzuri katika kumalizia.

Nafasi ya mwisho

Jambo jingine ambalo linaipasua kichwa Yanga ni kitendo cha kuburuza mkia katika msimamo wa ligi ikiwa haina pointi.

Kitendo cha Yanga kushika nafasi ya mwisho kimeibua mjadala ambao unaweza kuwatoa mchezoni wachezaji kama hawakuandaliwa vyema kisaikolojia.

Kauli za makocha

Pamoja na changamoto hizo, Zahera alisema Polisi Tanzania ni timu nzuri ambayo Yanga inapaswa kucheza kwa tahadhari wakati Matola alisema wanacheza na Yanga bila kuangalia rekodi za nyuma kwa kuwa mchezo wa soka una mabadiliko makubwa hivi sasa.